Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Kenya William Ruto wamezungumza kwa njia ya simu mapema hii leo na kujadiliana masuala mbalimbali yakiwemo ya kiusalama kati ya nchi hizo mbili na ushirikiano wao wa kudumisha usalama nchini Haiti.
Nchi hizo mbili pia zilizungumzia fursa za ziada za kukuza usalama wa kikanda na ustawi wa pamoja kwa kuchochea uwekezaji mpya, kazi na ukuaji endelevu.
Kulingana na taarifa kutoka White House, suala la vikosi vya ulinzi lilitawala mazungumzo kati ya viongozi hao wawili.
Wawili hao walikaribisha, kura iliyofanikiwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuidhinisha ujumbe wa usalama maarufu MSS kufikisha misaada ya ulinzi kwa watu wa Haiti.
Rais Joseph R. Biden, Jr. alizungumza na Rais William Ruto wa Kenya leo kumshukuru kwa kujibu wito wa Haiti wa kuhudumu kama taifa litakaloongoza ujumbe wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa (MSS).
Wakati huo huo, rais Ruto, amesema kuwa Marekani imeipongeza Kenya kwa kukubali kutuma vikosi vyake Haiti ili kurejesha utulivu kwa raia wa nchi hiyo na pia kwa kufanikiwa kuandaa mkutano wa tabia nchi barani Afrika.
Rais Ruto, aliandika kwenye mtandao wa X, kuwa uhusiano kati ya Kenya na Marekani unazingatia upanuzi wa ustawi wa pamoja wa nchi hizo mbili.
"Tutaendelea kushirikiana katika usalama wa kikanda, utatuzi wa migogoro na mapambano dhidi ya ugaidi ili kuhakikisha pembe ya Afrika ina nafasi ya kuzingatia maendeleo ya kijamii na kiuchumi." Ruto aliandika kwenye mtandao wa X.
Rais Biden aliishukuru Kenya kwa kukubali kuongoza ujumbe wa Msaada wa Usalama Wa Kimataifa (MSS) Kwenda Haiti na kueleza msaada wa Marekani kwa ujumbe huo.
Mazungumzo kati ya wawili hao yanajiri siku moja tu baada ya Rais Ruto kutetea uamuzi wa nchi yake kutuma askari wake nchini Haiti.