Polisi wa Ufaransa waliwakamata takriban watu 1,311 kote nchini huku maandamano ya vurugu kuhusu mauaji ya kijana yakiendelea kwa usiku wa nne, Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema Jumamosi.
Takriban maafisa 45,000 wa polisi wakiungwa mkono na magari ya kivita walitumwa kuzima maandamano hayo, ambayo ni pamoja na kuchoma moto dampo, magari na kuharibu majengo.
Kulingana na wizara hiyo, maafisa 79 wa usalama wakiwemo polisi na askari walijeruhiwa usiku kucha.
Nahel M, kijana mwenye umri wa miaka 17 mwenye asili ya Afrika Kaskazini, alipigwa risasi na afisa wa polisi siku ya Jumanne katika kitongoji cha Paris cha Nanterre.
Afisa huyo anakabiliwa na uchunguzi rasmi wa mauaji ya hiari na amewekwa katika kizuizi cha awali.
Umoja wa Mataifa pia umeelezea wasiwasi wao kuhusu mauaji ya polisi, na kuitaka Ufaransa kushughulikia "maswala mazito ya ubaguzi wa rangi na ubaguzi" katika vyombo vyake vya sheria.