Pakistan: Mahakama yasema kukamatwa kwa Imran Khan ni kinyume cha sheria

Pakistan: Mahakama yasema kukamatwa kwa Imran Khan ni kinyume cha sheria

Vyombo vya Habari vinaripoti kuwa mahakama hiyo imeagiza Khan kuachiliwa bila masharti
imran Khan, aliyekuwa waziri wa Pakistan Picha : Reuters / Photo: Reuters Archive

Mahakama ya juu zaidi nchini Pakistan imeamuru kuachiliwa mara moja kwa aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan.

Vyombo vya habari nchini Pakistan vimeripoti kuwa mahakama hiyo imeiagiza tume ya kukabiliana na ufisadi iliyomfungulia mashtaka Bwana Khan kumuachilia bila masharti na kutaja kukamatwa kwake kuwa ukiukaji wa haki na sheria.

maandamano Pakistan kufuatia kukamatwa kwa Imran Khan Picha : TRT World 

Kukamatwa kwa Khan Jumanne kulizua rabsha kati ya wafuasi wa Khan na wanajeshi waliotumwa kudhibiti maandamano, katika mikoa ya Punjab na Khyber Pakhtunkhwa, inayoaminiwa kuwa ngome kuu zake.

Ripoti zinasema kuwa watu tano wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa katika makabiliano hayo yaliyosababisha uharibifu mkubwa ikiwemo kuchomwa kwa magari na nyumba za serikali.

Kesi ya Khan iliyosikilizwa Jumatano katika majengo yasiyokuwa ya mahakama, iliishia kwa kukutwa na hatia ya ufisadi kufuatia shutuma za kuuza zawadi za serikali na kuficha zawadi alizopokea badala ya kuwasilisha kwa hazina kuu ya taifa.

Wafuasi wa Imran Khan wanadai kuwa mashtaka haya yamefunguliwa kama njama ya kumzuia kushiriki uchaguzi baadaye mwaka huu.

TRT Afrika