Mlipuko wa lori katika Miragoane nchini Haiti ulijeruhi takriban watu 40, huku wengine wakipata majeraha ya moto sehemu kubwa ya miili yao. / Picha: AP

Lori la mafuta lililipuka Jumamosi kusini magharibi mwa Haiti, na kuua watu 24, mamlaka ilisema, huku mashahidi wakiripoti kwamba waathiriwa walikuwa wakijaribu kukusanya mafuta yaliyokuwa yakivuja kutoka kwa gari hilo.

Mlipuko wa Miragoane ulijeruhi takriban watu 40, huku wengine wakipata majeraha ya moto sehemu kubwa ya miili yao, Emmanuel Pierre, mkuu wa wakala wa ulinzi wa raia wa Haiti, aliambia AFP.

Idadi ya waliofariki iliongezeka kutoka 16 mapema siku hiyo, baada ya waokoaji kugundua miili iliyoungua karibu na eneo la mlipuko, Pierre alisema.

Waliojeruhiwa walisafirishwa hadi Hospitali ya Sainte Therese katika mji wa bandari wa Miragoane, takriban kilomita 100 (maili 60) magharibi mwa mji mkuu Port-au-Prince.

Mkutano wa dharura

Sita baadaye walihamishwa hadi katika hospitali maalum huko Port-au-Prince.

Wengine 13 ambao awali walikuwa wamepangiwa kuhamishwa watasalia Miragoane kwa sababu kuungua kwa zaidi ya 80% ya miili yao kulifanya usafiri usiwezekane.

Waziri Mkuu wa muda Garry Conille aliitisha mkutano wa dharura wa serikali ili kukabiliana na janga hilo, Pierre alisema.

Haiti imekuwa ikikumbwa na ukosefu wa utulivu kwa miaka mingi na mji mkuu wake umechukuliwa na magenge ya wahalifu.

Ziara ya Blinken

Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Anthony Blinken alifanya ziara ya nadra mnamo Septemba 5, ambapo aliahidi msaada wa dola milioni 45 na kusisitiza haja ya uchaguzi, ambao haujafanyika nchini Haiti tangu 2016.

Blinken pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu mustakabali wa muda mrefu wa kikosi cha polisi kinachoongozwa na Kenya, ambacho kiliwasili miezi miwili iliyopita na kimepewa jukumu la kuleta utulivu katika Port-au-Prince na kwingineko.

TRT Afrika