Taarifa za kuuawa kwake zimethibitshwa na maafisa wa ulinzi nchini Ecuador licha ya video fupi za tukio la mauaji hayo kuenea mitandaoni kwa kasi.
Mpaka sasa bado uchunguzi unaendelea, maafisa wa usalama wanataja huenda ikawa ni shambulio lililopangwa.
Mkosoaji mkubwa wa serikali iliyo madarakani
Villavicencio, alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa ufisadi na uhalifu unaopangwa, alikuwa katika hafla ya kampeni siku ya Jumatano 9 Agosti, na wakati amemamliza mkutano na kujiandaa kuondoka ndipo alifyatuliwa risasi mara 3 zilizompata kichwani na kuchukua uhai wake papo hapo.
Villavicencio, ameuawa huku kukiwa na ongezeko la ghasia katika taifa linalolaumiwa kwa kufumbia macho walanguzi wa dawa za kulevya.
Mirindimo 30 ya risasi yasikika
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa risasi 30 zilipigwa kwenye tukio kaskazini mwa mji mkuu Quito.
Picha za video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha Villavicencio akiingia kwenye gari baada ya mkutano kumalizika, kabla ya sauti ya risasi na mayowe kusikika.
Siku 3 maombolezo, Uchaguzi upo pale pale
Rais anayemaliza muda wake Guillermo Lasso alithibitisha kuwa polisi walilipua kwa usalama guruneti lililoachwa nyuma na wauaji.
"Huu ni uhalifu wa kisiasa, ambao una tabia ya ugaidi, na hatuna shaka kuwa mauaji haya ni jaribio la kuhujumu mchakato wa uchaguzi," Lasso alisema katika taarifa yake ya video.
Lasso alitangaza siku 3 za maombolezo na hali ya hatari ya kitaifa, akisema jeshi litajipanga kuhakikisha usalama.
Lakini mbali na tukio hili kwa mujibu wa Rais Lasso mchakato wa uchaguzi wa kumchagua Rais uliopangwa kufanyika tarehe 20 Agosti utaendelea kama kawaida.
9 wajeruhiwa katika majibizano ya risasi
Ofisi ya mwanasheria mkuu ilisema mshukiwa mmoja wa uhalifu alifariki baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata katika majibizano ya kufyatua risasi. Katika tukio hilo jumla ya watu 9 walijeruhiwa, akiwemo akiwemo mgombea ubunge na polisi wawili.
Fernando Villavicencio alikuwa mwanasiasa wa Ecuador, mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi na mwanahabari ambaye alikuwa anawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2023 nchini humo.
Alihudumu kama mjumbe wa Bunge la Kitaifa kuanzia mwaka 2021 hadi kuvunjwa kwa chombo hicho cha kutunga sheria tarehe 17 Mei 2023.