Makundi mbalimbali ya Wapalestina yamekubali kumaliza migawanyiko yao na kuimarisha umoja wa Wapalestina kwa kutia saini Azimio la Beijing nchini China, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China.
Tamko hilo lilitiwa saini katika hafla ya kufunga mazungumzo ya maridhiano kati ya makundi yaliyofanyika Beijing kuanzia Julai 21-23, shirika la utangazaji la serikali CCTV lilisema Jumanne.
Jumla ya makundi 14 ya Wapalestina wakiwemo viongozi wa makundi hasimu ya Fatah na Hamas pia walikutana na vyombo vya habari, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi akiwapo, CGTN ilisema katika chapisho la mtandao wa kijamii.
Pande hasimu za Hamas na Fatah zilikutana nchini China mwezi Aprili kujadili juhudi za upatanisho ili kumaliza takriban miaka 17 ya mizozo.