Ukumbi maarufu wa Atlas Cinema wa mjini Istanbul ulifurika siku ya Jumamosi mchana kushuhudia uzinduzi wa makala ya uchunguzi ya “Holy Redemption”, inayoangazia namna walowezi wa Kiyahusi wanavyowaondoa Wapalestina kutoka makazi yao katika eneo la West Bank.
Jopo la wataalamu lilijadili mambo mbalimbali ya mapambano ya Wapalestina kabla ya onesho la kwanza la makala ya uchunguzi iliyofanywa na waandishi wa habari wa TRT World mwezi Disemba mwaka jana.
"Makala ya Holy Redemption sio tu kwamba inafichua yale ambayo yamefichwa kutoka kwa mtazamo wa ulimwengu lakini pia inaangazia mojawapo ya mbinu mbaya za uvamizi duniani," alisema Mehmet Zahid Sobaci, Mkurugenzi Mkuu wa TRT.
“Gaza imeteketezwa mbele ya macho yetu, huku baadhi ya mataifa yakiendelea kuwa kimya. Sisi, kama TRT, tutaendelea, kadiri ya uwezo wetu kuangazia vita vya Israeli katika eneo la Gaza.”
Waandishi wa TRT World wamejaribu kuziba pengo la namna ya kuripoti udhalimu wa walowezi haramu wa Israeli katika vijiji vya Wapalestina.
Timu yetu ya uchunguzi ya TRT imepata mafanikio makubwa ya uandishi wa habari kwa kupenyeza katikati vikundi vya Wazayuni wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi, miezi miwili tu baada ya Oktoba 7, makala hii ilirekodiwa katika mazingira magumu sana, huku wakihatarisha maisha yao,” alisema Omer Faruk Tanriverdi, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Matangazo ya Kimataifa wa TRT.
"Uzinduzi huu unakuja wakati muafaka. Serikali ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu inakabiliana na shinikizo baada ya walowezi wa Kiyahudi kuwashambulia wanakijiji wa Kipalestina katika eneo la Jit, Agosti 15.
"Israeli inajaribu kutekeleza utakaso wa kikabila kwa sababu kuna mzozo wa idadi ya watu kwa Waisraeli ambao kwa sasa unapendelea Wapalestina," alisema Sami Al-Arian, Mkurugenzi wa Kituo cha Uislamu na Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Istanbul Zaim.
"Wapalestina peke yao hawawezi kusambaratisha miundo hii dhalimu ya ukuu na ubaguzi wa rangi. Uthabiti wao na kukataa kwao kuondoka katika eneo hilo kuna nafasi yake, lakini kila mtu ana sehemu ya kutekeleza katika kukomesha dhuluma hii."
Makala hii muhimu inatoa mwonekano wa ukatili unaofanywa na walowezi wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kufichua athari za vitendo hivi kwa jamii za Wapalestina.
Filamu hiyo iliyorekodiwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa baada ya mauaji ya halaiki ya Gaza kuanza Oktoba 7, inaangazia madai ya walowezi kupata msaada kutoka kwa taifa na jeshi la Israeli.
Makala hii inasimulia masimulizi ya kutisha ya ugaidi na wizi wa ardhi unaofanywa na walowezi wenye itikadi kali dhidi ya Wapalestina, na kutoa mitazamo kutoka kwa wahusika na mashahidi wa matukio haya.
Kitendo cha kuionesha simulizi ya 'Holy Redemption' kwa umma wa kimataifa, "Ukombozi Mtakatifu" kinatafuta kuangazia mzozo unaoendelea katika eneo hilo na athari zake.
Akizungumza kabla ya kuoneshwa kwa filamu hiyo, mwanaharakati wa haki za binadamu Issa Amro, amesema kumekuwepo na ongezeko la vitendo vya ukatili vya Waisraeli dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi toka kuanza kwa vita hivyo, Oktoba 7.
“Kipindi hiki ni cha joto na hatuna maji ya kunywa,” alisema wakati akizungumzia ubaguzi ambao Wapalestina wanakabiliana nao kila siku. Walowezi wa Israeli wamepewa huduma za maji, mara 10 zaidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi, alisema.
"Makala kama hii husaidia kufichua ufashisti wa Israeli."
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na waandishi wa habari, wanaharakati, na wasomi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, pia ilishuhudia wataalam wakizungumza kuhusu mauaji ya kimbari ya Israeli dhidi ya Wapalestina na athari pana za vitendo hivyo.
Mwanahistoria mashuhuri wa Israel na mwanasayansi wa kisiasa Ilan Pappe alisema Wapalestina hawapaswi kukata tamaa mbele ya uchokozi wa taifa la Israeli.
"Mradi wa kikoloni wa walowezi unaanza kujidhihirisha, lakini unahitaji msaada mkubwa na hatua za kukomesha serikali ya ubaguzi wa rangi."
Filamu hiyo inaangazia eneo la pili lenye giza na kimya kwa kiasi kikubwa la vita - walowezi haramu wa Kizayuni wakiiba ardhi ya Wapalestina chini ya kivuli cha mauaji ya Israeli huko Gaza, ambayo yameua Wapalestina 40,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Katika kufanikisha kurekodi filamu hiyo, timu ya "Holy Redemption" ilikutana na wanaharakati wa Israeli na wanachama wa Knesset na kujipenyeza katika vikundi vya walowezi wa Kiisraeli wenye itikadi kali, wakiwemo Vijana mashuhuri wa Hilltop.
"Filamu hii ni muhimu sana kwa sababu katika Bunge la Marekani, tunasikia mara kwa mara kwamba tatizo lilianza Oktoba 7, na hii inaonyesha kwamba tatizo lilianza kabla ya hapo," alisema Medea Benjamin, mwanaharakati wa amani wa Marekani.
"Na ndio maana ningependa kuipeleka kazi hii mbele Congress ili kuionesha kwao."
Filamu hiyo ya TRT World imehusisha mahojiano ya kina. Inafichua mawazo ya kikoloni ya Israeli na ajenda iliyoratibiwa vyema kati ya watendaji wa serikali na magenge ya Kiyahudi yenye silaha ambao wana nia ya kuwalazimisha Wapalestina kuziacha nyumba za mababu zao katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Robert Martin, mwanaharakati wa Australia anayeunga mkono Palestina, alisema kwamba wakati Israeli inajaribu kujinasibu kama kinara wa demokrasia ulimwenguni, ukweli hauko hivyo.
“Kiuhalisia, Israeli ni taifa la kibaguzi”.