"Shirika la Hilal Nyekundu katika kila nchi, hufanya kazi kwa pamoja na wengine, na kupata nguvu katika nyanja ya misaada ya kibinadamu." amesema Yilmaz. / Picha : AA

Shirika la Hilali Nyekundu la Uturuki limefungua ofisi mpya ya uwakilishi katika mji mkuu wa Syria Damascus, ikiwa ni misheni yake ya pili ya kimataifa.

Ofisi hiyo ilizinduliwa katika makao makuu ya Hilali Nyekundu ya Syria (SARC) wakati wa hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Hilali Nyekundu wa Uturuki Fatma Meric Yilmaz, Rais wa Hilali Nyekundu wa Syria Mohammad Hazem, na Mkurugenzi Mkuu wa Hilali Nyekundu wa Uturuki wa Masuala ya Kimataifa na Huduma za Uhamiaji Alper Kucuk, pamoja na viongozi wengine siku ya Jumamosi.

Baada ya hafla ya kukata utepe na kutiwa saini kwa itifaki, ofisi ya ujumbe wa Uturuki ilianzishwa rasmi ndani ya jengo la Hilali Nyekundu ya Syria.

Misaada iligawanywa kwa wale wanaohitaji kufuatia tukio hilo. Yilmaz na Hazem baadaye walisafiri hadi wilaya ya Barzeh huko Damascus kupeleka misaada kwa wakazi wahitaji.

Yilmaz amemkabidhi Hazem tuzo ya ukumbusho, akimpongeza kwa kuteuliwa hivi karibuni kama rais wa Hilali Nyekundu ya Syria.

Alielezea kuridhishwa kwake na ushirikiano wao unaoendelea, akibainisha kazi yao ya awali juu ya juhudi za kibinadamu huko Idlib. Ofisi hii ya wajumbe itawasaidia kutathmini vyema mahitaji na kuratibu huduma katika eneo, Yilmaz alidokeza.

"Hilali Nyekundu ya kila nchi, kushirikiana na mashirika mengine ndani ya nchi yake, hupata nguvu kubwa katika utoaji wa misaada ya kibinadamu."

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo, na kuongeza: "Kama viongozi wa Hilali Nyekundu, tumeahidi kushirikiana katika kuharakisha juhudi za uokoaji na kuendeleza usaidizi wa kibinadamu."

Bashar al Assad, kiongozi wa serikali ya Syria kwa karibu miaka 25, alikimbilia Urusi baada ya makundi yanayopinga utawala kuchukua udhibiti wa Damascus Desemba 8, na kumaliza utawala wa Chama cha Baath, ambacho kilikuwa madarakani tangu 1963.

Unyakuzi huo ulikuja baada ya vikosi vya upinzani vya Syria kuteka miji muhimu katika mashambulizi ya kasi yaliyochukua chini ya wiki mbili.

TRT World