Jumamosi, Julai 20, 2024
2051 GMT - Mshauri wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House Jake Sullivan amesema Rais Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu watajadili njia za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika Gaza iliyozingirwa na kurejea kwa mateka wakati wa mkutano wao.
"Lengo kuu la mkutano kati ya Rais Biden na Waziri Mkuu Netanyahu litakuwa juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na mpango wa mateka," Sullivan aliambia Jukwaa la Usalama la Aspen huko Colorado.
Alisema Biden ataelekeza nguvu zake na Netanyahu "kufanya makubaliano haya katika wiki zijazo."
2248 GMT - Jeshi la Israeli laua kijana wa Kipalestina kusini mwa Ukingo wa Magharibi
Jeshi la Israel limemuua kijana wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Televisheni ya Palestina ilisema Ibrahim Zaqeeq, 19, alipigwa risasi kichwani na wanajeshi wa Israel huko Beit Ummar.
Ilisema Zaqeeq aliachiliwa kutoka jela ya Israel wiki mbili zilizopita na ndiye mtoto wa kiume pekee katika familia yake.
Walioshuhudia wameliambia Shirika la Anadolu kwamba jeshi la Israel lilivamia Beit Ummar na kuwafyatulia risasi Wapalestina, na kuwajeruhi vibaya Zaqeeq na wengine ambao walipoteza pumzi kutokana na gesi ya kutoa machozi.
2125 GMT - Maandamano yazuka Tunisia, Morocco dhidi ya mauaji ya Israeli huko Gaza
Maandamano ya kupinga mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza iliyozingirwa yalifanyika nchini Tunisia na Morocco na kuwavutia maelfu ya waandamanaji.
Katika mji mkuu wa Tunisia wa Tunis, waandamanaji walikusanyika kwenye barabara ya Habib Bourguiba kwa maandamano ya Mshikamano na Palestina.
Waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za Palestina na Tunisia waliimba nara kama vile "Uhuru kwa Palestina" na "Ulimwengu wa kinafiki umechoma moto Gaza na Palestina."
Maandamano kama haya yalifanyika katika miji kote Morocco, ikijumuisha Rabat, Fez, Meknes, Tangier, Kenitra, Nador, Ahfir, Taroudant na Agadir.
Maelfu walishiriki kuitaka Israel isitishe mashambulizi yake dhidi ya Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.