Amnesty International imeiasa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuichunguza Israeli kwa mauaji ya Wapalestina 44, wakiwemo watoto 32.
Wiki iliyopita, mwendesha mashtaka wa ICC Karim Khan, aliomba kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na kiongozi mkuu wa Hamas kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu.
Amnesty ilisema mashambulizi matatu ya Israeli- moja kwenye kambi ya wakimbizi ya al-Maghazi katikati mwa Gaza mnamo Aprili 16, na mawili huko Rafah kusini mwa Gaza mnamo Aprili 19 na 20 - "ni ushahidi zaidi wa muundo mpana wa uhalifu wa kivita" uliofanywa na Israeli huko Gaza.
"Kesi zilizoandikishwa hapa zinaonesha mfano wa wazi wa mashambulizi katika kipindi cha miezi saba iliyopita ambapo jeshi la Israeli limekiuka sheria za kimataifa, na kuua raia wa Palestina bila kuadhibiwa kabisa na kuonesha kutojali maisha ya binadamu," alisema Erika Guevara-Rosas, mkurugenzi mkuu wa Amnesty.