Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom anasema hali katika eneo la Gaza inaendela kuzorota.
Mashambulizi ya Isarel dhidi ya Gaza yameendela tangu Oktoba tarehe 7, baada ya mashambulizi ya kushtukiza ya Hamas.
"Kwa wastani, mtoto mmoja anauawa kila baada ya dakika 10 huko Gaza," Adhanom ameambia mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa wa baraza la amani na usalama.
Mkutano huo umejadili kuhusu hali ya Israel na ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
"Pia ninaelewa hasira, huzuni na woga wa watu wa Gaza, ambao tayari walikuwa wameteseka kupitia miaka 16 ya vizuizi, na sasa wanavumilia uharibifu wa familia zao, nyumba zao, jamii zao na maisha waliyoyajua," Adhanom ameongezea.
Mkurugenzi huyo amesema hali Gaza "haiwezi kuelezeka".
"Sakafu za hospitali zimetapakaa majeruhi, wagonjwa, na maiti,chumba cha kuhifadhia maiti kinafurika, upasuaji unafanyika bila dawa ya kuzuia uchungu yaani anesthesia," Adhanom ameelezea mkutano huo.
Zaidi ya watu 10,800 sasa wameuawa huko Gaza, karibu 70% yao wakiwa wanawake na watoto.
"Zaidi ya wanawake 180 hujifungua huko Gaza kila siku. Kuna wagonjwa elfu tisa wanaohitaji matibabu ya saratani. Na kuna wagonjwa elfu 350 wenye ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu," Adhanom amesema.
WHO inasema kuwa wiki iliyopita, ilinukuu mashambulizi 5 kwenye hospitali 5 kwa siku moja.
Adhanom amesema katika muda wa saa 48 pekee zilizopita, hospitali nne zenye vitanda 430 zimeharibiwa.
Zaidi ya wahudumu wa mashirika 100 wa Umoja wa Mataifa wameuawa.