Hotuba ya waziri huyo ilihusu ukosoaji wa muda mrefu wa Uturuki kwa kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua katika mgogoro wa Gaza. / Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, ameonya kwamba binadamu wapo karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote na "mgongano wa tamaduni."

"Hatujawahi kuwa karibu hivi na mgongano wa tamaduni kwa hali halisi," Fidan alisema Jumanne katika Mkutano wa 10 wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Muungano wa Tamaduni (10th UN Alliance of Civilisation Initiative Meeting) uliofanyika nchini Ureno.

Fidan alikosoa kuongezeka kwa chuki, misimamo mikali, chuki dhidi ya wageni, na ubaguzi wa rangi duniani, akibainisha mauaji ya halaiki ya Wapalestina huko Gaza yanayofanywa na Israeli kuwa mfano mbaya zaidi wa matatizo haya, na akatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kulishughulikia suala hilo.

Waziri huyo alieleza kuwa chuki inachochewa kwa makusudi kote ulimwenguni, akionya kuhusu hatari za kutokuchukua hatua.

"Kadri tunavyonyamaza, ndivyo mfumo wa kimataifa unavyozidi kugawanyika," alisema, akisisitiza madhara makubwa ya kupuuza mwenendo huu.

Akizungumzia vifo vya raia huko Gaza kutokana na mashambulizi makali ya Israeli kwa muda wa miezi 14, Fidan alisema hakutakuwa na amani iwapo njaa, umasikini, na vifo vitaendelea Gaza.

Aliitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kupunguza mateso ya Wapalestina na kuzuia hali zaidi ya kudhoofika katika eneo hilo.

Hotuba ya waziri huyo ilisisitiza ukosoaji wa muda mrefu wa Uturuki kwa kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu mgogoro wa Gaza, na mwito wake mpana wa mshikamano wa kimataifa dhidi ya mgawanyiko unaoongezeka.

TRT Afrika