Mwakilishi wa Uturuki katika Umoja wa Mataifa, Sedat Onal, amesisitiza haja ya lazima na ya haraka ya mageuzi ya Baraza la Usalama, akisema mchakato wa mageuzi unahitaji kushughulikia mapungufu ya sasa ya Baraza hilo.
"Haja ya mageuzi ya Baraza la Usalama ni jambo linalofaa kuungwa mkono na haliwezi kuepukika," Onal alisema Jumanne kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama.
"Kilichojiri hivi karibuni katika Baraza la Usalama kinathibitisha ukweli huu," alisema, akielezea kushindwa kwa Baraza hilo kuanzisha usitishaji vita na kusitisha mateso ya kibinadamu huko Palestina "kutokana na ulemavu wake wa asili."
Akisisitiza kuwa mchakato wa mageuzi hayo unahitaji kushughulikia na kuondoa kasoro zilizopo sasa za Baraza, mjumbe huyo alisema:
“Lazima liwe na malengo ya uwakilishi wenye usawa na kidemokrasia na yale ya ufanisi bila kuacha lengo moja kwa ajili ya jengine."
"Hii inahusisha ushirikishi ambao ungefaidika kwa kupata uungwaji mkono wa nchi zote wanachama. Njia moja ambayo itasisitiza na kutanguliza manufaa ya wote badala ya maslahi ya taifa moja," aliongeza.
Uhalali wa baraza unaangaziwa
Pia akizungumza katika mjadala wa kila mwaka, rais wa Baraza Kuu la UN Dennis Francis alisema kuwa bila marekebisho ya kimuundo, utendaji na uhalali wa Baraza utaendelea kuharibika.
"Vurugu na vita vinaendelea kuenea duniani kote, wakati Umoja wa Mataifa unaonekana kuwa dhaifu kutokana na mgawanyiko katika baraza la usalama," aliongeza.
Baraza la Usalama lilipitisha azimio kuhusu mzozo huo siku ya Jumatano, kufuatia majaribio manne ambayo hayakufanikiwa tangu yalipozuka mapema mwezi Oktoba.
Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Uturuki, zinaamini kwamba mageuzi katika Baraza la Usalama ni ya dharura zaidi kuliko hapo awali.
Katika hali hii, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito mara kwa mara wa mageuzi hayo.