Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis wamekutana kujadili mahusiano ya Uturuki na Ugiriki pamoja na masuala ya kimataifa ikiwemo mzozo unaoendelea Gaza.
Wakati wa mkutano huo uliofanyika kando ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumanne, Erdogan alimuambia Mitsotakis: "Uturuki na Ugiriki zinaweza kusonga mbele kwa hatua za kujiamini kuelekea siku zijazo kwa msingi wa ujirani mwema."
"Rais Erdogan alidokeza kuwa kuimarisha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili na kutenda kwa mujibu wa maneno na roho ya Azimio la Athens kutazinufaisha nchi zote mbili," kulingana na taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Erdogan na Mitsotakis walikubaliana kufanya mkutano wa Baraza la Ushirikiano wa Ngazi ya Juu kati ya nchi hizo mbili huko Uturuki mapema 2025.
Azimio la Athens
Uturuki na Ugiriki zilitangaza "Azimio la Athens juu ya Mahusiano ya Kirafiki na Ujirani Mwema" wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mji mkuu wa Ugiriki mnamo Desemba 2023.
Kwa mujibu wa tamko hilo, nchi hizo mbili zimesisitiza kuwa zimejitolea kukuza uhusiano wa kirafiki, kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na maelewano na kutafuta suluhu la mzozo wowote kati yao kwa kuzingatia sheria za kimataifa.
Kutokana na hali hii, walikubali kushiriki katika mashauriano endelevu yenye kujenga na ya maana kwa kuzingatia mazungumzo ya kisiasa, ajenda chanya na hatua za kujenga imani, na kujiepusha na vitendo na kauli ambazo zinaweza kudhoofisha moyo wa azimio.