Uturuki ina "matumaini zaidi kuliko hapo awali" kuhusu ununuzi wake wa F-16 kutoka Marekani, Rais Recep Tayyip Erdogan amesema.
"Matarajio yetu ni kwamba tutafikia matokeo chanya. Nina matumaini zaidi kuliko hapo awali (kuhusu suala hili)," Erdogan aliuambia mkutano wa wanahabari Jumatano mwishoni mwa mkutano wa NATO katika mji mkuu wa Lithuania Vilnius.
Kuhusu kukabiliana na ugaidi, alisema kuendelea na mapambano dhidi ya ugaidi ni muhimu kwa Uturuki.
"Tunatarajia msimamo thabiti na wazi kutoka kwa washirika wetu kuhusu suala hili," aliongeza.
Kuhusu uchomaji moto wa Quran nchini Sweden, kiongozi wa Uturuki alisema kuwa kushambulia maadili matakatifu ya watu sio uhuru wa kujieleza , akiita "unyama, upumbavu, na aina ya kitendo cha kigaidi."
Nchi ambazo zilipiga kura kupinga azimio la kulaani kitendo cha kuchomwa moto kwa Quran katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa "zinapaswa kufikiria upya" uelewa wao wa uhuru na haki za binadamu, alihimiza.
Siku ya Jumanne, Uingereza, Marekani na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilikataa kulaani kuchomwa moto kwa Quran wakati wa mjadala wa dharura katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Hii ilifuatia kuongezeka kwa idadi ya mashambulizi dhidi ya kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu.
Sera ya NATO ya kupokea kila mtu
Kuhusu ombi la Sweden kujiunga na NATO, Erdogan alisema:
"Bunge Kuu la Uturuki litapiga kura kuhusu itifaki ya Uswidi kujiunga na NATO. Manaibu wetu watafuatilia suala hilo kwa karibu."
Aliongeza: "Uturuki daima imekuwa ikiunga mkono sera ya NATO ya kupokea kila mtu. Hatujawahi kuzuia nchi yoyote kujiunga na muungano huo kwa sababu zisizo na msingi."
Pia akigusia mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi unaosimamiwa na Ankara, ambao unatazamiwa kumalizika Julai 17, kiongozi wa Uturuki alisema kuwa Ukraine inataka kuongeza muda wa makubaliano hayo na juhudi zinaendelea kushughulikia "mapendekezo ya Urusi."
"Iwapo Urusi na Ukraine zitatoa au kukubali upatanishi, Uturuki itafurahia kukubali ," Erdogan alisema.