Siku ya Jumamosi, Herzog alighairi ushiriki wake katika mkutano huo, akitaja "maswala ya usalama," kulingana na taarifa kutoka ofisi yake. / Picha: Jalada la AA

Uturuki imekataa ombi la Rais wa Israel Isaac Herzog la kutumia anga yake kwa safari yake ya ndege kuhudhuria mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP29 huko Baku, mji mkuu wa Azerbaijan.

Maafisa walithibitisha kuwa mamlaka ya Israeli iliwasilisha ombi la ndege ya Herzog kuvuka anga ya Uturuki ikielekea kwenye Mkutano wa 29 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. Hata hivyo, mamlaka ya Uturuki ilikataa ombi lake.

Siku ya Jumamosi, Herzog alighairi ushiriki wake katika mkutano huo, akitaja "maswala ya usalama," kulingana na taarifa kutoka ofisi yake.

Uhusiano kati ya Uturuki na Israeli umekuwa ukidorora tangu kuanza kwa mashambulizi mabaya ya Israeli dhidi ya Gaza kufuatia shambulio la kuvuka mpaka la kundi la Hamas la Palestina Oktoba 2023.

Mashambulizi yanayoendelea hadi sasa yamewauwa karibu watu 43,800 na kufanya eneo hilo kuwa karibu kutokuwa na makazi.

Takriban asilimia 90 ya wakazi wa eneo hilo wamekimbia makazi yao, huku wengi wakilazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa.

Mashambulizi ya Israeli pia yameharibu karibu theluthi mbili ya nyumba na majengo mengine huko Gaza, kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa.

Israeli pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa hatua yake katika eneo lililozingirwa.

TRT World