Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kushoto) akimkaribisha kiongozi wa kundi la Hamas la Palestina, Ismail Haniyeh (kulia), wakati wa mkutano wao kwenye Ikulu ya Rais mjini Ankara, Julai 26, 2023.

"Ninalaani vikali na kukana hadharani mauaji ya kiuhaini ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran," Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema, kufuatia mauaji ya Israel ya Haniyeh.

"Mauaji haya ni kitendo cha madharau kinacholenga kudhoofisha kadhia ya Palestina, ukakamavu uliotukuka wa Gaza, na mapambano ya haki ya ndugu zetu wa Palestina, kwa nia ya kuwakatisha tamaa na kuwatia hofu," Erdogan alisema Jumatano.

"Madhumuni ya mauaji haya ni sawa na mashambulizi ya awali ya Sheikh Ahmed Yassin, Abdulaziz El Rantisi, na watu wengine wengi wa kisiasa kutoka Gaza; hata hivyo, ukatili wa Kizayuni utashindwa tena kufikia malengo yake kama ilivyokuwa hapo nyuma," alisema.

'Uturuki itaendelea kuunga mkono Palestina'

Rais Erdogan pia alitoa wito kwa ulimwengu wa Kiislamu na mshikamani wa kibinadamu kuungana dhidi ya "ugaidi wa Israeli".

Erdogan amesema, kwa misimamo imara zaidi ya ulimwengu wa Kiislamu na mshikamano wa kibinadamu, ukandamizaji na mauaji ya halaiki huko Gaza na ugaidi unaoenezwa na Israeli katika eneo letu utafikia mwisho, na eneo letu na dunia itapata amani.

"Kwa lengo hili, Uturuki itaendelea kuchunguza njia zote, kutumia juhudi zote, na kusaidia ndugu zetu wa Palestina kwa uwezo na nguvu zetu zote. Tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kuanzishwa kwa taifa huru, na utawala wa Palestina, na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake, kwa kuzingatia mipaka ya 1967," Erdogan alisema.

"Ninaomba rehema kutoka kwa Mungu kwa ajili ya ndugu yangu aliyeuawa kishahidi Ismail Haniyeh, subira kwa ajili ya familia yake, na kutoa pole kwa ndugu zetu wa Gaza, Palestina, na ulimwengu wa Kiislamu."

"Mungu amjaalie pepo kwa rehema yake."

Fahrettin Altun, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki, pia amelaani vikali mauaji ya Ismail Haniyeh.

Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X, Altun alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Haniyeh, pamoja na watu wa Palestina.

"Namuombea rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu shahidi Ismail Haniyeh na rambirambi zangu kwa familia yake, watu wa Gaza, Palestina na ulimwengu wa Kiislamu," alisema.

Rais wa Uturuki Erdogan na maafisa wengine wakuu wa Uturuki wamekutana na mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh mara kadhaa tangu mashambulizi ya Israeli dhidi ya Wapalestina kuanza Oktoba mwaka jana.

Shahidi kwa ulimwengu wote wa Kiislamu

Msemaji wa Chama cha AK Omer Celik amesema kuwa kifo cha kishahidi cha Haniyeh, kutokana na kujitolea maisha yake yote kwa kadhia ya Palestina, kinapita zaidi ya huzuni ya sasa hivi ya watu wa Palestina.

"Haniyeh ni shahidi sio tu kwa Wapalestina bali kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu," Celik alisema.

Celik alisisitiza kuwa Netanyahu na timu yake wanatekeleza mauaji ya kimbari ambayo hayajawahi kutokea huko Gaza. Aliongeza kuwa waliona dalili kwamba Netanyahu atatumia Oktoba 7 kupanua vita katika eneo hilo.

TRT World