Takriban watu 200,000 watafaidika na misaada hii. / Picha: AA

Shirika la msaada lenye makao makuu mjini Istanbul liliwasilisha kontena 15 zenye vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa Sudan kupitia meli.

Kupitia taarifa yake, Shirika hilo la misaada la Kibinadamu la IHH lilisema kuwa vyakula, bidhaa za usafi, na blanketi zilitumwa Sudan kwa njia ya bahari. Iliongeza kuwa takriban watu 200,000 watafaidika na misaada hiyo.

Sudan imekumbwa na mvutano kati ya jeshi la Sudan na wanajeshi wa kitengo cha Rapid Support Forces (RSF) tangu Aprili, kwenye mzozo ambao umesababisha vifo vya raia 3,000 na kujeruhi maelfu, kulingana na wataalam wa afya katika eneo hilo.

Licha ya juhudi kadhaa za kusitisha mapigano na kuleta upatanishi iliyosimamiwa na wapatanishi wa Saudia na Marekani kati ya mahasimu hao wanaozozana, ghasia hizo hazijaweza kukomeshwa.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa karibu watu milioni 3 wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo nchini Sudan.

Mapema mwezi huu wa Julai, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alionya kwamba mzozo unaoendelea nchini Sudan huenda ukaingia katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.

Kukimbia mzozo

Zaidi ya watu milioni 4 wamesalia kuwa wakimbizi nchini Sudan, wakiwemo milioni 2.5 wa ndani kwa ndani na milioni 2.2 katika nchi jirani, kulingana na UN.

Mapigano nchini Sudan tangu Aprili 15 yamesababisha mmiminiko wa watu waliokimbia nchi hiyo kuelekea mataifa jirani, yakiwemo Misri, Chad, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa maendeleo zaidi ya mzozo nchini Sudan yanaweza kuyumbisha eneo kubwa zaidi.

AA