Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amezungumza kwa njia ya simu na rais wa Mali Assimi Goita na kuzungumzia ushirikiano kuhusu suala la mapambana dhidi ya ugaidi na masuala mengine.
"Wakati wa maongezi hayo, uhusiano wa nchi mbili kati ya Uturuki na Mali, ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi, na masuala ya kikanda na kimataifa yalijadiliwa," kulingana na taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki katika siku ya Jumatano.
Erdogan alielezea azma ya Uturuki ya kuendeleza ushirikiano na Mali katika sekta afya, nishati, kilimo, viwanda, teknolojia, elimu na biashara, taarifa hiyo ilisema.
Aliitaka Mali kuchukua hatua kukomesha shughuli za Shirika la Kigaidi la Fetullah (FETO) nchini humo na kuwarejesha wanachama wake Uturuki.
FETO na kiongozi wake aliyoko Marekani Fethullah Gulen waliandaa mapinduzi yaliyoshindwa ya Julai 15, 2016, huko Uturuki, ambapo watu 252 waliuawa na 2,734 kujeruhiwa.
Erdogan pia alisisitiza uungaji mkono wa Uturuki kwa Mali katika kupambana na ugaidi na kudumisha amani na utulivu wa kikanda.
Mali imekuwa ikipambana na uasi unaohusishwa na ugaidi wa Al Qaeda na Daesh tangu mwaka 2012 wakati machafuko yalipozuka kaskazini mwa nchi hiyo.