Rais Erdogan ametoa salamu za rambirambi kwa njia ya simu alipozungumza na Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber. / Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber na kutoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian.

"Wakati wa maongezi ya simu hiyo, Rais Erdogan alieleza masikitiko yake kwa kupoteza Rais wa Iran Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian, pamoja na ujumbe aliofuatana nao katika ajali mbaya ya helikopta, na kuwasilisha rambirambi zake na kuwataka wawe na subra," Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema kupitia mtandao wa X siku ya Jumatatu.

"Kwa kuzingatia kwamba Uturuki inasimama upande wa Iran katika siku hizi za uchungu na inashiriki huzuni ya watu wa Iran, Rais Erdogan alisema kuwa Uturuki itaendelea kutekeleza wajibu wa ujirani na udugu kwa Iran katika kipindi kijacho," kurugenzi hiyo iliongeza.

Michango ya Raisi na Amirabdollahian katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili itakumbukwa daima, rais wa Uturuki alisema.

Baada ya msako wa usiku mzima uliotatizwa na hali mbaya ya hewa, Raisi, Amirabdollahian na maafisa wengine wakuu wametangazwa kufariki.

Makumi ya timu za uokoaji za dharura zilikuwa zimetumwa kwenye eneo la milimani kaskazini magharibi mwa mkoa wa Azerbaijan Mashariki mwa Iran, ambapo kisa hicho kilifanyika Jumapili alasiri.

Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, makamu wa kwanza wa rais Mohammad Mokhber, atachukua mamlaka ya urais na uchaguzi utafanyika ndani ya siku 50.

TRT World