Rais wa Serbia Aleksandar Vucic ameipongeza Uturuki kama nchi yenye nguvu ya kuleta utulivu katika Balkan na kuelezea matarajio yake ya kuendelea kwa uungwaji mkono wa Uturuki wa amani katika eneo hilo.
Akizungumza pamoja na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Serbia siku ya Ijumaa, Vucic alisisitiza kuwa Uturuki inaongoza kama nchi yenye "nguvu kubwa zaidi katika Balkan."
Erdogan yuko Belgrade kama sehemu ya ziara yake nchi za Balkan. Uturuki na Serbia zilitia saini mikataba 11 ya makubaliano inayohusisha sekta mbalimbali kutoka kwa nishati hadi mawasiliano.
"Mahusiano yetu ya kiuchumi na kibiashara yanaunda injini ya ushirikiano wetu wa nchi mbili na Serbia. Kiwango chetu cha biashara kimevuka dola bilioni mbili kwa miaka miwili mfululizo," Erdogan alisema katika hotuba yake, akiongeza kuwa lengo sasa limewekwa kuwa dola bilioni tano.
Alisema kuwa Uturuki na Serbia pia zina fursa za kuimarisha ushirikiano wa sekta ya ulinzi na kuzitaka nchi ambazo hazihusiani na mkataba huu kujiepushe na kujaribu "kuamua ni nini sekta ya ulinzi ya Uturuki na Serbia" inapaswa kufanya.
Mahusiano yanaendelea vizuri
Erdogan alisisitiza zaidi "umuhimu wa mbinu ya kujenga ya Serbia katika kusaidia Bosnia na Herzegovina kusonga mbele zaidi ya udhaifu wake wa kisiasa.
"Rais wa Serbia, kwa upande wake, pia alimsifu Erdogan kama mtu ambaye "anaelewa vizuri matatizo ya Balkan na daima anasema kuwa mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuyatatua."
Vucic alisema sehemu za Serbia zimesaidika kutokana na uwekezaji wa Uturuki na alionyesha kuthamini kwa nchi yake uhusiano wa kirafiki na Uturuki - nguvu muhimu ya kisiasa na kiuchumi huko Eurasia na ulimwengu wote.
Uturuki inaiona Serbia kama nchi muhimu kwa utulivu katika eneo hilo na inaunga mkono ushirikiano wake na EU, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki.
Uturuki pia inaona uhusiano na Serbia ukiendelea vyema, huku ziara za pande zote mbili za ngazi ya juu na uhusiano wa kibiashara na kiuchumi ukiendelea kwa kasi kubwa.