Katika ziara hio Waziri Hakan Fidan pia anatarajiwa kukutana na wafanya biashara Wakituruki huko Urusi. /Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, atasafiri hadi Urusi kwa ziara ya siku mbili ili kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya BRICS na nchi nyingine kadhaa, kwa mujibu wa duru za kidiplomasia.

Vyanzo hivyo vilisema Fidan atahudhuria mkutano huo katika mji wa Nizhny Novgorod siku ya Jumanne na kufanya mazungumzo na maafisa wa Urusi akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov.

Majadiliano yatazingatia masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na matukio ya hivi karibuni huko Gaza, Ukraine, Syria, Libya, na Caucasus Kusini.

Fidan atasisitiza matarajio ya Uturuki ya kupatikana kwa amani na kusitishwa vita vinavyoendelea katika eneo lake haraka iwezekanavyo, pamoja na nia yake ya kutoa msaada katika mwelekeo huo, vyanzo vilisema.

Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara pia uko kwenye ajenda, ikijumuisha juhudi za kuongeza uwekezaji wa pande zote, na kufikia lengo la kiasi cha biashara cha dola bilioni 100, lililowekwa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Katika ziara hiyo, Fidan pia anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wa Uturuki wanaofanya kazi nchini Urusi.

Mkutano wa BRICS

Mkutano wa Jumanne utaangazia masuala ya usalama wa kimataifa, maendeleo endelevu, na utawala wa kimataifa, huku BRICS ikizikaribisha nchi 15 zisizo wanachama kuhudhuria, Uturuki, Bahrain, Bangladesh, Belarus, Algeria, Indonesia, Kazakhstan, Cuba, Laos, Mauritania, Nigeria, Thailand, Sri Lanka, Venezuela, na Vietnam.

Fidan pia anatarajiwa kufanya mikutano na nchi zingine pembezoni mwa mkutano huo.

Rais Erdogan pia alikuwa ameshiriki katika Mkutano wa 10 wa BRICS mjini Johannesburg mwaka 2018.

Urusi ilichukua uenyekiti wa BRICS kutoka Afrika Kusini kufikia Januari 1, ikipitisha kaulimbiu, "Kuimarisha ushirikiano wa nchi nyingi kwa maendeleo ya haki ya kimataifa na usalama."

Mkutano wa 16 wa kilele wa BRICS umepangwa kufanyika Kazan mnamo Oktoba 22-24.

TRT World