Mke wa Rais wa Uturuki Emine Erdogan amempongeza mshindi wa tuzo ya Nobel Muhammad Yunus baada ya kuapishwa kuwa rais wa serikali ya mpito ya Bangladesh kufuatia machafuko ya wiki kadhaa nchini humo.
"Napenda kumtakia heri Mheshimiwa Prof. Muhammad Yunus, mwanachama wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa ya Watu Mashuhuri ya Kukabiliana na Uchafuzi wa Mazingira, ambayo nimepata heshima ya kuwa mwenyekiti, anapoanza jukumu lake jipya la kiongozi wa Serikali ya Mpito ya Bangladesh," Mke wa Rais alisema katika taarifa kwenye mtandao wa X, ambayo zamani ilifahamika kama Twitter, siku ya Alhamisi.
Yunus amekua rais wa serikali ya mpito baada ya ghasia za wanafunzi kumlazimisha Waziri Mkuu wa zamani Sheikh Hasina kujiuzulu na kukimbilia India.
Rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin alimuapisha Yunus siku ya Alhamisi kwa nafasi yake kama mshauri mkuu, ambayo ni sawa na nafasi ya waziri mkuu, wakiwa mbele ya wanadiplomasia wa kigeni, wanachama wa mashirika ya kiraia, wafanyabiashara wakuu na wanachama wa chama cha zamani cha upinzani katika Ikulu ya rais huko Dhaka.
Emine Erdogan pia alionyesha imani katika uwezo wake wa kuchangia pakubwa demokrasia, amani na utulivu nchini Bangladesh.
"Nawatakia watu wenye urafiki na undugu wa Bangladesh kila la heri."
Watu wengine kumi na sita wamejumuishwa katika Baraza la Mawaziri la muda na wanachama kutoka kwa mashirika ya kiraia na wakiwemo viongozi wawili wa maandamano ya wanafunzi.
Wajumbe wa Baraza la Mawaziri walichaguliwa baada ya majadiliano wiki hii kati ya viongozi wa wanafunzi, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wanajeshi.
Hasina alijiuzulu Jumatatu baada ya wiki kadhaa za machafuko ambazo zilianza Julai na maandamano dhidi ya mfumo wa upendeleo wa kazi za serikali ambao wakosoaji walisema unapendelea watu wenye uhusiano na chama cha Hasina.
Lakini maandamano hayo hivi karibuni yalikua changamoto kubwa kwa utawala wa miaka 15 wa Hasina, kwani zaidi ya watu 300 wakiwemo wanafunzi waliuawa huku kukiwa na vurugu zikiendelea.