Katika mkutano huo, Erdogan na Al Thani pia walijadili uhusiano kati ya mataifa hayo mawili pamoja na masuala ya kimataifa na kikanda. /Picha: AA

Rais wa Uturuki kwa mara nyingine tena ameitaka jumuiya ya kimataifa kukomesha ongezeko la hatari la Israeli la uvamizi wake wa kijeshi, akionya kwamba inaweza kuliingiza eneo hilo katika mgogoro mkubwa na mbaya zaidi.

Katika mkutano na Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara, Recep Tayyip Erdogan amesema Tel Aviv inajaribu kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo kupitia mashambulizi yake katika maeneo ya Palestina na Lebanon, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema katika taarifa.

"Rais Erdogan alisema kwamba kuuawa kwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh na Israeli, kwa mara nyingine tena yamedhihirisha ukosefu wa nia ya Israeli ya kusitisha mapigano."

Israeli haijakiri hadharani kumuua Haniyeh katika shambulizi mjini Tehran wiki iliyopita, lakini ripoti zinasema kuwa Tel Aviv ndio waliohusika na mauaji hayo na hata waliifahamisha Marekani kuhusu hilo.

Erdogan alisema Uturuki inafanya juhudi za kuleta amani ya kudumu katika eneo hilo na itafanya kazi kwa karibu na Doha ili kufikia lengo hilo.

Katika mkutano huo, Erdogan na Al Thani pia walijadili uhusiano kati ya mataifa hayo mawili pamoja na masuala ya kimataifa na kikanda.

Akielezea "dhamira kamili" ya Uturuki ya kuendeleza ushirikiano wake na Qatar katika uhusiano wa kiuchumi, na vile vile katika nyanja za kisiasa, kijeshi, kibiashara na kitamaduni, rais wa Uturuki alisema hatua za siku zijazo zitaimarisha mshikamano kati ya nchi hizo mbili.

TRT World