Rais wa Uturuki Erdogan alijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya sala ya Ijumaa. /Picha: AA

Marekani na Uingereza zimetumia nguvu zisizo na uwiano nchini Yemen, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya swala ya Ijumaa mjini Istanbul, Erdogan alikosoa mashambulizi dhidi ya Yemen yaliyofanywa na Marekani na Uingereza.

"Hatua hizi zote zinahusisha matumizi ya nguvu zisizo na uwiano. Israel pia inatumia nguvu zisizo na uwiano huko Palestina," alisema. "Tunapokea taarifa kutoka kwa vyanzo mbalimbali kwamba Houthis wamejilinda kwa mafanikio makubwa, na kutoa majibu yenye mafanikio dhidi ya Marekani na Uingereza," alisema.

Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi kwenye shabaha nyingi ndani ya Yemen mwishoni mwa Alhamisi kujibu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Houthis kwenye njia za kimataifa za meli katika Bahari Nyekundu.

Mashambulizi ya kundi la Yemen yalianza mwezi Novemba kujibu hujuma za Israel dhidi ya Wapalestina tangu tarehe 7 Oktoba.

Kesi ya mauaji ya kimbari ya Afrika Kusini

Kuhusu kesi ya mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, Erdogan alisema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hana pa kujificha na kwamba hakuna utetezi kwa matendo yake.

"Nilimuona Rais (wa Israeli) (Isaac) Herzog katika hali ya dhati zaidi wakati huu, lakini hivi majuzi, pia amemuiga Netanyahu, akianza kutoa kauli tofauti," aliongeza.

Alibainisha Israel inawasilisha hoja zake katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa na kuongeza: "Lakini nyaraka ambazo tumewasilisha ni muhimu kwa The Hague."

Siku ya kwanza ya kesi hiyo ilihitimishwa Alhamisi baada ya Balozi wa Afrika Kusini nchini Amsterdam, Vusimuzi Madonsela, kusoma hatua tisa za muda ambazo nchi yake iliomba kutoka kwa Mahakama dhidi ya Israel. Katika siku ya kwanza ya kesi hiyo, upande wa Afrika Kusini uliwasilisha mashtaka yao dhidi ya Israel kwa ICJ pamoja na sababu na ushahidi.

Wawakilishi wa kisheria wa Afrika Kusini katika kesi hiyo waliishutumu Israel kwa "vitendo vya makusudi dhidi ya wakazi wa Gaza, kuthibitisha nia ya mauaji ya kimbari."

TRT Afrika