Wakati wa mkutano wao, Fidan na Abdelatty watajadili maandalizi ya mkutano wa kwanza wa Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa Ngazi ya Juu, utakaofanyika wakati wa ziara ijayo ya Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi nchini Türkiye. / Picha: Jalada la AA

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan anatazamiwa kuanza ziara ya siku mbili nchini Misri siku ya Jumapili kwa mwaliko wa mwenzake wa Misri Badr Abdelatty, kwa mujibu wa duru za kidiplomasia.

Uhusiano kati ya Ankara na Cairo hivi karibuni umeona maendeleo makubwa. Ziara rasmi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini Misri mnamo Februari 14, ikiwa ni ziara ya kwanza katika ngazi hiyo katika kipindi cha miaka kumi na mbili, iliashiria hatua kubwa katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, tamko la pamoja lilitiwa saini kwenye kikao cha Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa Ngazi ya Juu kilichoongozwa na marais wa nchi hizo.

Mwezi uliopita, Badr Abdelatty aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Misri katika serikali mpya iliyoundwa. Ziara inayokuja itaashiria mkutano wa kwanza rasmi wa Fidan na mwenzake wa Misri.

Wakati wa mkutano wao, Fidan na Abdelatty watajadili maandalizi ya mkutano wa kwanza wa Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa Ngazi ya Juu, utakaofanyika wakati wa ziara ijayo ya Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi nchini Uturuki.

Pia watatathmini hali ya sasa ya takriban mikataba 20 inayotarajiwa kutiwa saini wakati wa mkutano huo.

Majadiliano hayo yatahusu mahusiano ya nchi mbili za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, pamoja na maendeleo ya sasa ya kikanda. Fursa za ushirikiano wa muda mrefu katika nishati, afya, utalii, na sekta ya ulinzi pia zitajadiliwa.

Mada kuu za ziara hii ni pamoja na maendeleo ya Gaza, suala la Palestina, misaada ya kibinadamu kwa Gaza, na kuongezeka kwa mvutano wa kikanda. Zaidi ya hayo, maendeleo katika Libya, Sudan, na Somalia yatatathminiwa.

Fidan anatarajiwa kuzuru Al-Arish na mpaka wa Rafah kuingia Gaza na kukagua kituo cha usafirishaji cha Hilali Nyekundu cha Misri ambacho kinashughulikia usafirishaji wa misaada ya kibinadamu kutoka Uturuki hadi Gaza.

TRT World