Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameangazia jukumu la msaada wa Marekani katika kuwezesha matendo ya Israel huko Gaza, ambayo yamesababisha mauaji ya kimbari.
Hakan Fidan aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na kituo cha habari cha Uturuki NTV siku ya Jumatano alipokuwa akizungumzia sera za kigeni.
Akiashiria tofauti ya kimsingi katika msimamo kati ya Uturuki na Marekani kuhusu vita vya Gaza, Fidan alisema Marekani inaiunga Israeli mkono bila masharti huko Gaza wakati Uturuki imeiunga mkono Palestina bila masharti tangu mwanzo.
Alisema ni muhimu kwa dola kuweza kutofautisha migogoro na ushirikiano katika mahusiano yake na mataifa mengine huku akibainisha kuwa Ankara na Washington pia zinashirikiana katika baadhi ya maeneo kama vile NATO na baadhi ya masuala ya teknolojia.
"Katika suala la Gaza, katika suala la Palestina, haiwezekani kwa Israeli kuchukua hatua kwa ujasiri kama huo, kutekeleza mauaji ya halaiki, bila uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa usio na masharti wa Amerika. Marekani inawezesha hili,” alisema.
'Suluhu ya nchi mbili ndio njia pekee'
Fidan pia alikiri kwamba Ankara na Washington kwa sasa wanakubaliana juu ya umuhimu wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na utoaji wa haraka wa msaada wa kibinadamu katika eneo lililozingirwa.
Fidan alisema pia wanakubaliana kuwa bila suluhu ya nchi mbili, suala hilo litaendelea kuwa tatizo la mara kwa mara.
Kuhusu kesi ya mauaji ya halaiki iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israeli katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, alidokeza kuwa Afrika Kusini ndiyo nchi inayofaa zaidi kufanya hivyo kwa sababu ya historia yake ya kuushinda utawala wa kibaguzi na ubaguzi wa rangi na kuwa wamepitia ukandamizaji.
Israeli imeshambulia Gaza kufuatia shambulio la kundi la Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana ambalo liliua takriban watu 1,200.
Zaidi ya Wapalestina 35,200 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na zaidi ya 79,000 wamejeruhiwa, kulingana na mamlaka ya afya ya Palestina.
Katika Ukingo wa Magharibi (West Bank) unaokaliwa kwa mabavu, karibu Wapalestina 500 wameuawa na maelfu kujeruhiwa tangu wakati huo, pamoja na kukamatwa kila siku na jeshi la Israeli.
Israeli inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo imeiamuru Tel Aviv kuhakikisha kuwa vikosi vyake havifanyi mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inatolewa kwa raia huko Gaza.