Uturuki na Marekani zinahitaji kupitisha "mbinu za kimkakati" kushughulikia tofauti zao kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, Balozi wa Ankara mjini Washington amesema, wakati akihutubia Mkutano wa 39 wa Marekani na Uturuki mjini Washington.
"Licha ya hatua za kimaendeleo katika mahusiano yetu ya kiuchumi na hatua kuelekea mazungumzo ya kisiasa yaliyopangwa ndani ya muktadha wa utaratibu wa kimkakati, bado kuna nafasi ya kuboreshwa kwa masuala mbalimbali yenye utata katika mahusiano yetu ya nchi mbili," alisema Sedat Onal siku ya Ijumaa, ambayo ilikuwa ni siku ya pili ya mkutano huo.
Mkutano huo wa siku mbili umekuwa kama jukwaa kwa ajili ya wafanyabiashara wa Marekani na Uturuki kujihusisha na diplomasia ya kibiashara, na unaonesha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika masoko ya sekta za kimkakati.
"Ili kushughulikia tofauti zetu kwa njia inayofaa na yenye mwelekeo wa matokeo, tunahitaji kupitisha mbinu ya kimkakati, " Onal aliwaambia wahudhuriaji wa mkutano huo.
Ongezeko la ushirikiano kati ya Ankara na Washington kutaimarisha usalama, utulivu na ustawi na kuchangia katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu, aliongeza.
"Kukubali kutokubaliana na kukutana kwa kiwango cha chini kabisa cha kawaida hakuwezi na hakupaswi kutosha kwa washirika wa kimkakati," alisisitiza.
Mahusiano ya pande nyingi
Akisisitiza kwamba mahusiano ya Uturuki na Marekani pia yameathiriwa na historia, jiografia, tunu za ulimwengu, na maslahi ya kitaifa, Onal alisema kwamba mshikamano wa washirika hao wawili wa "NATO" umepitia mitihani mingi, hasa katika nyakati za Vita Baridi.
“Mahusiano yetu si ya sasa tu, bali yana siku za nyuma na yana siku za usoni na hatua tunayochukua inapaswa kuendana na hali hii ya mahusiano yetu yenye pande nyingi,” alisisitiza.
Akibainisha kwamba zinahitajika juhudi za dhati kwa kutilia maanani hisia za kila mmoja na masuala ya usalama yaliyopo, balozi huyo alihimiza mazungumzo "ya wazi na endelevu" ambayo yanajumuisha kuongezeka kwa mwingiliano sio tu katika ngazi ya serikali lakini pia katika bunge, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.
Onal pia alibainisha kuwa "machafuko ya kikanda yaliyotokana na mashambulizi ya Septemba 11 na vuguvugu la nchi za Kiarabu yameleta changamoto na tofauti" katika mahusiano ya Uturuki na Marekani.
"Kwa sasa, Uturuki, imezungukwa na maeneo mengi yenye vita na ukosefu wa utulivu, kutoka Syria hadi Iraq na Libya, Ukraine na Gaza," Onal alisema, akiongeza kuwa utatuzi endelevu wa migogoro hii unahitaji usawa kati ya wadau wakuu, kanuni na mazungumzo ya kidiplomasia.
"Muunganiko mkubwa na ukamilishano kati ya nchi zetu mbili bila shaka utaleta maana kubwa katika suala hili," aliongeza.
Balozi wa Marekani mjini Ankara, Jeff Flake, kwa upande wake alibainisha kuwa Uturuki na Marekani ni "washirika wa lazima," na akasisitiza kwamba "Uturuki daima itakuwa na jukumu muhimu la utekelezaji".
Aliongeza kuwa muungano wa Uturuki na Marekani umekuwa zaidi ya siasa za kijiografia kwani nchi zote mbili zinashirikiana tunu na maadili na maslahi ya pande zote.
"Tumethibitisha hilo katika miongo kadhaa tangu Vita vya Pili vya Dunia mara nyingi ambapo kanuni zetu za pamoja zimepingwa," Flake alisema.