Jude Bellingham akishangilia bao lake dhidi ya Serbia kwenye michuano ya fainali za mataifa ya Ulaya (Euro) 2024 inayoendelea kutimua vumbi nchini Ujerumani./Picha: Getty

Nyota wa Real Madrid Jude Bellingham aliihakikishia Uingereza alama tatu na uongozi wa kundi C kufuatia bao lake dhidi ya Serbia katika mchezo wao wa ufunguzi uliofanyika kwenye uwanja wa Veltins Arena.

Bellingham alifunga kwa kichwa katika dakika ya 13 ya mchezo huo, kufuatia kazi nzuri ya Bukayo Saka katika michuano ya fainali za mataifa ya Ulaya (Euro) 2024 inayoendelea kutimua vumbi nchini Ujerumani.

"Ni mwanzo mzuri kwangu na ninajisikia furaha kuipa timu yangu ushindi ambacho ni kitu muhimu zaidi kwa sasa," alisema Bellingham.

Hata hivyo, mchezo huo nusura uingie dosari kufuatia vurugu kati ya mashabiki wa pande hizo mbili, hatua iliyowalazimu walinda usalama kuingilia kati na kuwatenganisha.

Hapo awali, Denmark na Slovenia zilitoka suluhu ya 1-1, huku Christian Eriksen akiifungia Denmark, miaka mitatu tangu alipodondoka uwanjani kwa mshtuko wa moyo, katika mchezo wa kwanza wa kundi B wa michuano ya EURO 2020 kati ya Denmark na Finland.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika