Al Ahly Sporting Club ya nchini Misri imetangazwa kuwa klabu bora barani Afrika kwa mwaka 2024.
Mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara 12 wametwaa tuzo hiyo wakati wa halfa ya kuwatambua wachezaji wa Afrika waliofanya vizuri kwa mwaka 2024, iliyofanyika Disemba 16 jijini Marrakech nchini Morocco.
Mashetani hao wekundu kutoka Misri wanatwaa tuzo hiyo kwa mara ya saba, huku tuzo ya timu bora kwa upande wa wanawake ikienda kwa TP Mazembe.
Kwa upande wa walinda mlango, tuzo ya golikipa bora kwa upande wa wanaume ilienda kwa Ronwen Williams kutoka Afrika Kusini, wakati Mnigeria Chiamaka Nnadozie, alitwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.
Emerse Faé kutoka Ivory Coast alitangazwa kama kocha bora, wakati Lamia Boumehdi wa TP Mazembe akitwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.
Mbali na tuzo hizo, usiku huo pia ulichagizwa na burudani nzuri ya muziki kutoka Diamond Platnumz wa Tanzania, ambaye alikonga nyoyo za wahudhuriaji wa shughuli hiyo kupitia kwa wimbo wake Comment ça va.