Kulingana na kanuni za maandalizi za shirikisho la Soka barani Afrika ( CAF), wenyeji wa mashindano wanatakiwa kuwa na viwanja 6,/ Picha : TRT Afrika

Na Lynne Wachira

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Wadau kutoka Kenya , Uganda na Tanzania walijumuika kwa pamoja kwa Mara ya kwanza tangu mataifa hayo yalipokabidhiwa uenyeji wa MAKALA ya 36 ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka wa 2027.

Waziri wa Michezo wa Kenya, Ababu Namwamba aliandaa kikao cha siku mbili kusini mwa Pwani ya Kenya ili kuzungumzia jinsi mataifa yote matatu yataandaa mashindano kwa utangamano kwa Ushirikiano mkubwa.

"Michezo ni Chombo Chenye nguvu kubwa na ndiposa tunaendelea kujivunia kuwa wenyeji wa mashindano ya Soka ya hadhi ya juu zaidi barani Afrika,'' alisema waziri Namwamba. ''Bila shaka ni wakati wa Afrika mashariki kujitambulisha kama eno moja kupitia mchezo wa soka." aliongezea kusema huku akisisitiza kuwa ' Mataifa yetu yalistahili kuchaguliwa kama wenyeji."

Maandalizi ya viwanja

Kulingana na kanuni za maandalizi za shirikisho la Soka barani Afrika ( CAF), wenyeji wa mashindano wanatakiwa kuwa na viwanja 6, viwili vikiwa na uwezo wa kumudu idadi ya mashabiki wasiopungua elfu 40,000 na viwanja vinne visivyopungua mashabiki 20,000.

Licha ya kuunganishwa kupitia mipaka, mataifa yote Matatu yanakabiliana na Changamoto ya miundombinu haswa viwanja na ndio maana wanasema ujenzi na ukarabati wa viwanja utapewa kipau mbele.

Uganda imechagua uwanja wa Kimataifa wa Mandela unaofahamika zaidi kama Namboole kuwa uwanja wake mkuu/ Picha : TRT Afrika

"Kombe la mataifa ya Afrika ambalo linaorodhesha timu ishirini na nne linatwika wenyeji garama ya juu na ni vigumu kwa Taifa lolote kutoka Afrika mashariki kutimiza Matakwa yote ya CAF,” alikiri afisa wa shirikisho la kandanda nchini Uganda, Rogers Byamukana.

Uganda imechagua uwanja wa Kimataifa wa Mandela unaofahamika zaidi kama Namboole kuwa uwanja wake mkuu huku kazi ya ukarabati wa kuboresha kiwango cha Uwanja huo ikitazimiwa kuanza hivi karibuni,'' aliongeza bwana Rogers.

Uwanja wa Nakivubo ambao pia uko katika eneo la mji mkuu wa Kampala umeorodheshwa kama mwenyeji wa michuano ya AFCON huku Byamukana akisema kuwa, “ Uwanja huo wa Nakivubo umekuwa chini ya ukarabati kwa takriban mwongo mmoja na hatimaye unakaribia sana kukamilika .”

Wakati huo huo Uganda ilitangaza rasmi kuwa itajenga uwanja mpya wa kisasa katika eneo la Hoima, takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu Kampala.

“Inapendeza sana kuona serikali zote tatu zikijitolea na kujituma kutenga fedha ambazo zitatumika kujenga viwanja vipya kabisa, urithi wa kombe la dunia mwaka wa 2027 utakuwa viwanja vya kisasa ambavyo vitawezesha kuboresha viwango vya michezo mbali mbali kando na soka.” alisema bwan Rogers.

Uganda ilitangaza rasmi kuwa itajenga uwanja mpya wa kisasa katika eneo la Hoima, takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu Kampala. / Picha : TRT Afrika

Tutakuwa tayari, liwe liwalo – Waziri Namwamba

Sawia na Uganda Kenya pia itakarabati viwanja vyake vikubwa jijini Nairobi na vile vile uwanja wa Kipchoge Keino katika eneo la Rift Valley, takriban kilomita 300 kutoka mji mkuu wa Nairobi.

Tayari viwanja hivyo vitatu vitakarabatiwa chini ya uongozi wa idara ya jeshi kama njia mojawepo ya kuhakikisha vigezo vyote haswa muda wa kukamilisha vimezingatiwa, Waziri wa michezo wa Kenya Ababu Namwamba amethibitisha.

“Ningependa kuhakikishia bara nzima kuwa hakuna lolote litatokea kutatiza mipangilio tuliyoweka katika ujenzi na ukarabati wa viwanja, tutakuwa tayari miaka miwili kabla ya mashindano kungo’a nanga,” alisema waziri Namwamba.

Wakati huo huo, Kenya imetangaza ujenzi wa uwanja mpya kabisa utaofahamika kama Uwanja wa Talanta mjini Nairobi.

Tanzania afadhali zaidi lakini wanasaka kuboresha viwango

Iwapo mechi ya Ufunguzi ya kombe la dunia itachezwa hii leo, uwanja wa kimataifa wa Benjamin Mkapa ulioko mjini Dar es Salaam utakuwa chaguo bora zaidi kwani uko tayari.

Hivi majuzi, Uwanja huo unaoweza kumudu idadi ya mashabiki elfu 60,000 uliandaa sherehehe na mechi ya ufunguzi ya Ligi mpya kabisa ya Afrika ambayo inajumuisha baadi ya ya baadhi ya vilabu tajika nchini .

Vile vile ukarabiti unaendelea katika uwanja wa Uhuru katika manispaa ya Kinondoni na uwanja wa Major General Isamuhyo - viwaja hivi vimeratibiwa kukamilika mwezi ujao.

Kama ilivyo nchni Kenya na Uganda, Tanzania itajenga viwanja vipya kabisa katika mji wa Dodoma na Arusha/ Picha : TRT Afrika

Akizungumza katika kikao cha washikadau nchini Kenya, rais wa shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania, Wallace Karia alisema kuwa , “ Viwanja vyetu viko vizuri na tunasonga na ratiba yetu vilivyo.”

Kama ilivyo nchni Kenya na Uganda, Tanzania itajenga viwanja vipya kabisa katika mji wa Dodoma na Arusha – ujenzi umeratibiwa kuanza rasmi mwaka ujao.

“Tayari tumeweka mikakati itakayotuwezesha kukamilisha miradi hii muhimu, lakini muhimu zaidi ni kusonga mbele kwa pamoja na wenzetu Kenya na Uganda,” alidokeza Karia.

Kuweka dhamana kwa CAF

Karia pia alifichua kuwa Zanzibar itahusishswa kwenye maandalizi ya AFCON kama njia mojawepo ya kuhakikisha kuwa raha ya dimba hilo imesambaa katika maeneo mengi zaidi nchini.

Waziri wa michezo wa Zanzibar Tabia Maulid Mwita alihudhuria kikao hicho cha washikadau, “ Tuna furaha isiyo kifani kufahamu kuwa muungano wetu wa Tanzania ni wa kudumu, maandalizi tayari yameng'oa nanga haswa ukarabati wa uwanja wa Amaan ambao utakuwa mwenyeji wa baadhi ya mechi za Afcon.”

Kando na maandalizi ya viwanja, gharama ya mashindano ya mwaka wa 2027 haijabainika wazi.

Kulingana na kanuni mpya za shirikisho la Soka barani ( Caf), wenyenyeji wanahitajika kulipa kiasi Fulani cha pesa miaka miwili kabla ya mashindano kama ishara ya uwezo wa kifedha.

Kando na maandalizi ya viwanja, gharama ya mashindano ya mwaka wa 2027 haijabainika wazi./ Picha : TRT Afrika 

Kwa mfano, Kenya, Uganda na Tanzania wanatarajiwa kulipa bima ya dola milioni 90, ikiwa ni dola milioni 30 kila mmoja kufikia tarehe 15, Januari mwaka wa 2025.

Afisa wa shirikisho la soka la Uganda ambaye pia anasimamia kitengo cha mauzo na udhamini Rogers Byamukana anafafanua zaidi kuhusu fedha hizo, “ Wengi wanadhani fedha hizi zitarejeshewa serikali lakini sivyo kwani zitatumika kwenye maandalizi, malipo ya hoteli, usalama kati ya majukumu mengi ambayo huambatana na mashindano ya viwango vya juu.”

Ili kuendeleza maandalizi kwa pamoja bila mgawanyiko, kamati andalizi ikiwa na wawakilishi kutoka mataifa yote matatu itajumuishswa hivi karibuni.

TRT Afrika