Adama Bojang ‘The Hurricane’ anyakua nafasi adhimu katika historia ya FIFA

Adama Bojang ‘The Hurricane’ anyakua nafasi adhimu katika historia ya FIFA

Mshambuliaji huyo wa miaka 19, tayari ameibuka kuwa mchezaji nyota katika soka barani Afrika.
ADAMA BOJANG amekuwa nyota katika timu yake inayocheza kombe la dunia U20 Picha : AFP

Mshambuliaji wa Gambia Adama Bojang amejihakikishia nafasi katika kumbukumbu ya FIFA baada ya jezi yake kuchukuliwa na kutundikwa katika makavazi ya soka ya FIFA.

Shati la mchezaji huyo, nambari 20 mgongoni imewasilishwa kwa mkurugenzi wa mashindano wa FIFA anayesimamia eneo la Mendoza nchini Argentina, baada ya Young Scorpions hao kufuzu duru ya mchujo ya kombe la dunia U-20 inayoendelea.

‘'Jezi yangu inawekwa katika makavazi ya soka ya FIFA! Ni heshima kubwa sana kwangu.’’ Adama aliiambia TRT Afrika.

Kikosi cha Gambia cha wachezaji wasiozidi miaka 20 kimeonesha ustadi wa kipekee kujikomboa kutoka timu dhaifu zaidi wakianza duru ya makundi na kumaliza wakiwa juu kwa alama 7, wakilinganishwa tu na vigogo kama vile England na Argentina.

GAMBIA BOJANG ADAMA wa Gambia amesaidia timu yake kufika kilele cha jedwali katika duru ya makundi n ahivvyo kujitengea nafasi katika duru yu mchujo Picha : Timu ya taifa         

Akizungumza na TRT Afrika akiwa njiani kwenda kwenye mechi yao ya mchujo katika kombe la dunia U-20, Adama Bojang amesema, ''Nimefurahi sana kwasababu mimi ndiye raia wa kwanza wa Gambia kupata tuzo hii. Ni mafanikio makubwa kwangu na ninatoa shukrani kwa wachezaji wenzangu na kwa kocha wangu kwa juhudi zote ."

Matokeo haya yamesababisha jina la Bojang kuacha mwangwi katika uwanja hata baada ya mechi kumalizika. Bila shaka hili liliwavutia FIFA waliomtafuta kumpatia hadhi hii ya kufana kwa wachezaji.

Ikiwa na makao yake makuu mjini Zurich Uswisi, makavazi hayo ya soka ya FIFA ilizinduliwa 2016 kama kumbukumbu ya mafanikio, urithi na historia ya mchezo maarufu zaidi duniani.

FIFA imeandika katika mtandao wake kuwa, ''Makavazi hii itasaidia muungano wa kihisia unaowaleta pamoja wapenzi wa soka.''

Adama Bojang anaungana na magwiji wachache wa soka Afrika ambao jezi zao zimepata hadhi hii, akiwemo Asamoah Gyan wa Ghana, kwa umahiri wake wakati wa kombe la dunia 2010, pale nchi yake ilikosa kwa unywele tu kupenya kuweka historia kama taifa la pekee la Afrika kufika nusu fainali ya kombe la dunia.

Akizungumza na TRT Afrika kabla ya mechi yao ya mchujo Alhamis, Kocha Abdoulie Bojang, amesema soka ya Gambia inaendelea kukua. "Hii ni ishara wazi kuwa mchezo wa soka nchini Gambia imeshika mkondo sawa, na nimeridhishwa kuona mshambuliaji nyota wetu amepata jezi yake katika makavazi ya soka ya FIFA."

Mwingine ni beki wa Comoro Chaker Alhaddhur, ambaye alilazimika kuwa mlinda lango wakati wa mechi yao dhidi ya wenyeji Cameroon kombe la taifa bingwa Afrika Afcon 2022.

Adama Bijang Anajiandaa na timu yake kwa mechi ya mchujo dhidi ya Uruguay Picha : Timu ya Taifa Gambia 

Wengi waliandika pongezi zao za Bojang katika mitandao ya kijamii wakisema kuwa ameibuka kama mchezaji mwenye mwanga atakaye vunja mipaka katika soka Afrika.

TRT Afrika