Na
Nana Dwomoh-Doyen Benjamin
Kutokana na falsafa kubwa yenye mizizi iliyochanua ya falsafa ya kina ya Ubuntu – yenye msemo maarufu usemao "Nipo kwa sababu upo" - mpango huu unatafuta kuziba pengo kati ya Afrika na diaspora yake, kuendeleza uhusiano ambao kwa muda mrefu sana ulipotea.
Ubuntu Connect ni wito wa kuzidisha utambulisho wa Mwafrika katika mioyo na akili za Waafrika na ndugu, jamaa na marafiki ambao wamesambaa na waliotawanyika kote ulimwenguni.
Katika msingi wa Ubuntu Connect kuna ufahamu kwamba kila mwanadamu ameunganishwa kihalisi, si tu kwa jumuiya yao ya karibu, bali pia na mizizi ya mababu zao.
Kwa kukumbatia na kuishika falsafa ya Ubuntu, tunatambua kwamba hatima zetu zimeunganishwa, na tunalazimika kusaidiana na kuinuana, bila kujali mipaka ya kijiografia.
Sehemu ya kwanza ya Ubuntu Connect inaanza na kutilia mkazo katika taaluma, safari ya ugunduzi wa mambo mbalimbali.
Hii inajumuisha mfululizo wa mihadhara ya kuchanganua mambo mbalimbali ya kifikra ambayo inaangazia historia ya kabla ya ukoloni wa Afrika, athari kubwa ya biashara ya utumwa iliyovuka Atlantiki, utajiri wa mila, kanuni, sheria na hali ya kiroho ya Kiafrika.
Washiriki mbalimbali watapata uelewa wa kina wa urithi wao wa pamoja, na kukuza hali ya kujistahi na umoja.
Kupitia uzoefu wa vitendo, Ubuntu Connect itawaongoza washiriki kwenye maeneo ya urithi, ambapo wanaweza kutembea katika nyayo za mababu zao, wakifufua majaribio na dhiki za njia za watumwa zinazovuka Atlantiki.
Sio tu shughuli ya kitalii; ni uzoefu wa kihisia na mageuzi ambao huchochea uponyaji, upatanisho, na uvunjaji wa pingu za kihistoria na kupambana na utandawazi.
Mpango huu umeundwa kwa njia ya kipekee ili kuwatia moyo wanafunzi wa historia, imani za kidini za Kiafrika, na utamaduni kushuhudia mfanano wa kitamaduni na aina mbalimbali barani Afrika.
Wanaposimama kwenye udongo uleule kama mababu zao walivyofanya hapo awali, watatambua uzuri wa utambulisho wao wa pamoja na nguvu inayotokana na tofauti zao.
"Kuvumbua Uafrika Uliopo Katika ya Waafrika waliopo Afrika na waliosambaa duniani kote”. ndiyo mada ya programu hii ya kitaaluma na ya vitendo, inayowafikia Waafrika walio ng'ambo duniani kote.
Chama cha Wazalishaji Maudhui wa Afrika, kwa ushirikiano na taasisi kama vile Chuo Kikuu cha Afrika cha Mawasiliano na Mafunzo kilichopo nchini Nigeria, pamoja na watawala mbalimbali wa kitamaduni kote barani Afrika, wamechukua hatamu na wamekubali kuunga mkono mradi huu muhimu.
Mahusiano mazuri
Ili kuhakikisha uhifadhi na usambazaji wa historia na utamaduni wa Kiafrika, tafiti za kihistoria na za kitamaduni zitaanzishwa katika kila Jumba la Maonesho ya Kiafrika.
Hii sio tu itawezesha vizazi vijavyo kwa maarifa na hekima lakini pia kulinda asili ya Ubuntu kwa karne nyingi zijazo.
Ubuntu Connect imezua gumzo na kuleta mazungumzo ya shauku kutoka Liberia, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Cape Verde, Nigeria, Ghana, Zambia, na diaspora. Inasimama kama ushuhuda wa nguvu ya hatua ya pamoja na maono ya pamoja.
Wanadiaspora, kwa kaliba na utaalamu mbalimbali, wanahimizwa kuchangia katika kujenga uwezo wa ardhi ya mababu zao. Uhusiano huu wa maelewano utasababisha Afrika yenye ustawi, ambayo hutumia nguvu za jumuiya zake zilizotawanyika.
Afrika si tu chombo cha kijiografia, ni nchi ya kiroho na kihisia ambayo inakaa katika mioyo ya mamilioni ya watu duniani kote.
Ushindi wa mababu
Ubuntu Connect inalenga kuwasha upya mwanga wa kujiheshimu na kuwa ndani ya mioyo ya Waafrika, na kuwasha hamu ya kuchangia ukuaji na ustawi wa nchi yao na bara lao Mama
Mpango huu unatumika kama wito wa wazi kwa Waafrika wote, ndani na nje ya nchi, kuungana chini ya bendera ya Ubuntu na kushirikiana katika kujenga bara linalostawi.
Ubuntu Connect inawaalika Waafrika kutambua mapambano na ushindi wa pamoja wa mababu zao, unaowaunganisha pamoja katika historia na urithi.
Katika enzi ambapo uhifadhi wa kitamaduni na utambulisho ni muhimu zaidi kuliko hapo awali, Ubuntu Connect inasimama kama mwanga wa matumaini na njia ya kurejesha hali kuwa shwari.
Lengo kubwa la Ubuntu Ni kuthamini utofauti, ushindi wa umoja, na kujitolea kusaidiana katika kutafuta ukuu.
Roho ya kudumu
Wakati ulimwengu ukitazama Afrika kwa shauku kubwa kwa mustakabali wa bara hili, Ubuntu Connect inaashiria enzi mpya kwa Afrika na watu walio katika Diaspora .Hakika Hii ni hadithi ya uponyaji, upatanisho, na maendeleo.
Ni ushuhuda wenye nguvu wa uthabiti na roho ya kudumu ya Ubuntu ambayo inaishi ndani yetu sote.
"Kwa moyo wa Ubuntu, tuje pamoja, tukiwa tumeshikana mikono, kuanza safari hii ya kuleta mabadiliko. Kwa pamoja, tutaandika upya historia, tukiungana tena na mizizi yetu na kuweka msingi wa Afrika bora, iliyoungana zaidi - Afrika ambayo sio tu inatambua zama zake lakini, inayokumbatia mustakabali wake kwa mikono miwili. Mimi nipo kwa sababu wewe pia upo”.
Tahadhari: Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni, maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.