Na Omar Abdel-Razek
Michuano ya AFCON 2023 inayoendelea nchini Ivory Coast ni tukio kubwa sana barani Afrika. Hili sio jukwaa la mamilioni ya mashabiki kuzishabikia timu zao tu, lakini ni fursa ya kuangalia mchango wa baadhi ya wachezaji nyota wanaosakata kabumbu katika klabu tofauti barani Ulaya.
Majina kama Sadio Mané kutoka Senegal na Mohamed Salah wa Misri mifano hai ya muktadha huu. Hata hivyo, ni vyema kujiuliza kama wachezaji hawa wanawakilisha utandawazi katika soka la Afrika au kuchoka kwa vipaji?
Ingawa soka ndio mchezo maarufu zaidi barani Afrika, maendeleo yake ndani ya miongo michache iliyopita haijafikia umaarufu wake. Uwekezaji hafifu, ufisadi na kushuka kwa viwango wa baadhi ya wachezaji nyota ndio sababu ya anguko la soka barani Afrika.
Wachambuzi wengi wanaendelea kulinganisha kiwango cha soka barani Afrika na kile cha Ulaya: Hata hivyo ni kwanini soka la Afrika linaendelea kuporomoka wakati ndio fursa muhimu ya ajira, uwekezaji na pato la taifa kwa nchi nyingi barani Ulaya?
Mashirikisho yote mawili, yaani CAF kwa upande wa Afrika na UEFA kwa Ulaya, yametofautiana miaka mitatu toka kuanzishwa kwao. UEFA ilianzishwa mwaka 1954 na ina vyama 55 chini yake.
Kwa upande wake, CAF ilianzishwa mwaka 1957, ikiongozwa kwa mara ya kwanza kati ya Sudan, Ethiopia, na Misri, baada ya kujiondoa kwa Afrika ya Kusini kwa kususia kushirikisha timu zenye wachezaji wenye asili mbili tofauti.
Ikiwa na wananchama 54, mwaka 2023 CAF ilitangaza kuwa mapato yake yalifikia dola milioni 125.2.
Kwa upande mwingine, ripoti ya mwaka ya Deloitte ya mapato ya fedha yatokanayo na mchezo wa soka, ilionesha kuwa thamani ya soko la mpira wa miguu Ulaya lilifikia yuro bilioni 29.5 kwa mwaka 2022, huku ligi kubwa tano barani humo, zikichangia yuro bilioni 17.2.
Tofauti ya ulinganifu huu ndio inaweza kuelezea sababu ya wachezaji wengi wenye umri mdogo kutoka Afrika kukimbilia Ulaya.
Kuna zaidi ya wachezaji 500 kutoka bara la Afrika wanaosakata kabumbu katika baadhi ya ligi nchini Ulaya, ambayo ni sawa na asilimia 35 ya wachezaji kutoka nje katika timu kubwa barani humo.
Wengi watasema kuwa wachezaji hao wametangaza nchi zao na wamekuwa mifano ya kuigwa kwa watoto na vijana wanaosakam umaarufu na fedha. Huwezi kuukataa mchango wa Mo Salah katika kuzihuisha tunu hizi.
Wakati mashabiki wa Liverpool wakimuimba Mo Salah, kama zawadi kutoka kwa Allah” au hata wanapomlinganisha na mfalme wa Misri, ni dhihirisho tosha kuwa wachezaji wa namna hii wanaweza kuibadilisha dunia.
Kulingana na utafiti wa 2021 uliofanywa na chuo kikuu cha Stanford, uwezo wa Salah pamoja na imani yake umebadilisha taswira ya imani hiyo machoni na vichwani mwa mashabiki wa Liverpool.
Hoja nyingine yenye kutetea safari za wachezaji wa Afrika Ulaya ni ya kiutandawazi zaidi. Kwamba, katika dunia yenye uchumi uliotandaa, soka pamoja na wachezaji wake ni bidhaa zinazopaswa kuendana na mahitaji na matakwa ya soko.
“Uchovu wa wachezaji”
Ingawa uhamaji wa wafanyikazi, wenye ujuzi na wasio na ujuzi, kutoka nchi za pembezoni kama vile Afrika, Asia, na Amerika ya Kusini kwenda 'duniani' ulienea sana baada ya vita vya pili vya dunia, kuhama kwa wanasoka bado ni suala geni.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990s, klabu nyingi za Ulaya ziliondoa vikwazo katika idadi ya wachezaji wa nje watakaochezea klabu zao, baada ya Mahakama ya Ulaya kutoa hukumu yake kupitia sheria ya Bosman mwaka 1995.
Baada ya hukumu hiyo, ikawa ngumu zaidi kwa vilabu barani Afrika kuwazuia wachezaji wao wa ndani kutolea macho na udenda mikataba minono kutoka klabu kubwa Ulaya, kulingana na Iwebunor Okwechime na Olumide A. Adetiloye, kupitia utafiti wao uliochapishwa mwaka 2019.
Mwenendo kama huu ulitoa fursa kwa klabu kubwa Ulaya kuanzisha mitandao ya kusaka na kuvuta vipaji kutoka Afrika.
Mitandao hii ilihusisha mawakala, shule za michezo na wasaka vipaji ambao sio sehemu ya mfumo uliojaa ukiritimba na ufisadi, kama ule wa Afrika.
Kasoro za Kimuundo
Ni vyema kufahamu na kukumbuka hapa kwamba kilele cha uhamiaji wa mwanasoka kwenda Ulaya kilikuja katika kipindi cha msukosuko kwa nchi nyingi za Kiafrika.
Miaka ya 1990 ndio kipindi ambacho nchi nyingi za Kiafrika zililazimika kutekeleza mageuzi ya uliberali mamboleo yaliyowekwa na taasisi za fedha za kimataifa, ambayo ilimaanisha kuwa sekta kama vile michezo na utamaduni zilikuwa anasa kwa serikali nyingi za Kiafrika, na kusababisha wachezaji wenye vipaji na wengine kutafuta maslahi zaidi barani Ulaya.
Uzembe wa aina hii, sanjari na vitendo vya rushwa na upendeleo ndivyo vilipelekea soka la Afrika kudidimia.
Vilabu vingi vya Kiafrika vinaendeshwa na serikali, zenye rasilimali chache za kifedha, ukosefu wa viwanja, mafunzo, na shule za michezo zilizodhibitiwa kutengeneza na kulea vipaji vya soka. Wachezaji wengine wanalalamika kuwa hawapokei mishahara yao kwa miezi kadhaa.
Mchakato wa usajili wa wachezaji hauko wazi na hufuata maamuzi ya mawakala wa wachezaji na kiasi gani wanawalipa. Katika miaka ya hivi karibuni, ligi nyingi Ulaya zimekuwa zikitazamwa sana kuliko hata za ndani.
Hata idadi ya mashabiki wa ndani inazidi kushuka, hali inayowanyima klabu nyingi za ndani mapato kama klabu nyingi za Ulaya.
Licha ya uwepo wa wachezaji wengi wa Kiafrika duniani, kiwango cha mpira barani Afrika bado hakifanani na kile cha Ulaya au Marekani ya Kusini, isipokuwa kwa mataifa machache kama vile Afrika ya Kusini na Misri.
Uendeshwaji wa soka barani Afrika sio wa kiuweledi na hivyo kupelekea wachezaji wengi kuchoka mapema.
Ni muhimu sana kushughulikia kasoro za namna hii ili soka la Afrika liweze kupiga hatua kimataifa.
Uwepo mkubwa wa wanasoka wa Kiafrika kwenye hatua za kimataifa unakinzana na hali ya kuzorota ya mchezo katika ngazi ya ndani. Isipokuwa kwa wachache, kama vile Afrika Kusini na Misri, vilabu vingi vya Afrika vinafadhiliwa kidogo na viwanja duni na vifaa duni vya mazoezi.
Soka la Afrika linakosa weledi ulioinua viwango vya soka barani Ulaya na Marekani ya Kusini. Kama hazitofanyiwa kazi, basi bara la Afrika litashindwa kutimiza malengo yake ya kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2026, kutoka timu 5 hadi kufikia 9.