Jumatatu alfajiri mjini Istanbul, na nimeamshwa na king’ora katika simu yangu. Saa kumi na mbili unusu. Lakini sio siku ya kawaida. Tarehe mosi Mei ni sikukuu ya wafanyakazi kote duniani. Huko nje, kila kitu kimya.
Lakini nimejikuta nawaza juu ya kitu nilichokisoma mwishoni mwa wiki, juu ya kazi bora zaidi duniani. Kuna kitu kama hicho kweli?
Katika udadisi wangu, nikakutana na baadhi ya mifano. Kiukweli, baadhi ya kazi walizozitaja zilikuwa za kuvutia.
1. Mshauri wa chokoleti: Hii kweli ni kazi ? Sidhani kama ningelalamika katika kazi hii hata ingekuwa na mshahara duni. Kazi yao ni kuchambua aina bora zaidi ya Chokoleti, kutofautisha viwango kwa ubora wake na kupendekeza namna ya kutumia. Hii naweza kulinganisha na kazi ya waonja chai na kahawa.
2. Mhifadhi wa kisiwa - Hebu tulia kwanza. Yaani mimi nifanye kazi kwa bidii mwaka mzima, nihifadhi pesa na muda ili niweze kugharamia likizo, ambayo kwa mtazamo wangu likizo bora zaidi ni kubangaiza katika kisiwa nikinywa madafu. Lakini kumbe kuna mtu analipwa kufanya kazi hiyo?
3. Mtu anayelipwa kulala – Afadhali nijiepushe kutoa maoni yangu juu ya kazi hii. Bila shaka kuna sababu za kisayansi hasa kama wataalamu wa masuala ya usingizi wanaohitaji kufanyia uchunguzi mambo kama kulala vyema au ndoto. Lakini ni haki kweli uache kazi zingine zote na ulipwe sasa kulala tu?
Kuna kazi zingine nyingi tu ambazo ningefurahia sana kupewa. Hasa ikiwa zinahusisha kula, kusafiri au vitu ninavyopenda.
Lakini kwa upande mwingine, kuna baadhi ya kazi ambazo namuomba Mungu sana asinijaalie kufanya. Nilirudi katika mtandao kuangalia wanasemaje juu ya kazi mbaya au ngumu zaidi duniani.
1. Kazi ya chura – Yaani msafishaji vyoo na mabomba yake. Hii bila shaka ni miongoni mwa kazi muhimu duniani na ninawashukuru na kuwapongeza wote wanayofanya kazi hii. Lakini! Mimi Siwezi ifanya hii kazi.
2. Mchimba madini – Hii inanikumbusha mjomba wangu mmoja. Alikuwa akifanya kazi katika mgodi wa dhahabu na nilikuwa nikimuambia soini nikifanya kazi hiyo. Kwa mtazamo wake, mimi nilikuwa goigoi tu niliyehitaji kufanyishwa kazi ngumu. Miaka kadhaa baadaye, pole kumueleza kuwa bado siwezi kazi ya migodini.
3. Kazi ya vichinjio – Hebu tulia. Bado sijaanza kukataa kula nyama na kugeuka kuwa mla mboga. Japo naheshimu maoni yao hasa juu ya kupinga ukatili dhidi ya wanyama. Ukiona wakati mwingine mambo yanayofanyika machinjioni, unaweza kukinai. Lakini lazima kuwe na mtu wa kufanya kazi hiyo. Mimi naweza? La!
Watu wengi wametaja kazi ya kuhudumia maiti. Pengine kwa ajili mimi kama muislamu nimehusika mara kadhaa katika kusafisha maiti, kukafani na kisha kuzika, sina uoga wowote wa maiti. Naona naweza kuifanya kazi hii. Lakini naelewa kwanini wengine wanaogopa. Siku hizi hata kuna shahada zinafundishwa vyuoni za kuhudumia maiti.
Kimsingi nadhani muhimu zaidi ni iwapo unaipenda kazi yako. Baadhi ya kazi japo sio za kuridhisha, zina umuhimu zaidi. Haya ni maoni yangu. Najua mara nyingi tunaposikia juu ya kazi ya mtu mwingine tunaingiwa na tamaa kama tungepewa sisi. Lakini tahadhari,'' Usione chungu kipya ukatupa cha zamani.''