Mashabiki wamewasili, wachezaji wamewasili, mji wa Istanbul, nchini Uturuki uko tayari kwa mechi ya fainali ya kifahari zaidi ya soka barani Ulaya, kwa mara ya pili.
Manchester City na Inter Milan wanamenyana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Jumamosi mjini Istanbul huku timu ya Uingereza, chini ya Pep Guardiola, akiwa na imani kubwa ya kushinda tuzo kubwa zaidi ya vilabu vya Ulaya kwa mara ya kwanza.
Mechi hiyo itafanyika katika uwanja wa Olimpiki wa Atatürk, mjini istanbul wenye viti 75,000.
Timu ya Inter Milan inawania taji la kwanza la Barani Ulaya tangu 2010, wakati Jose Mourinho alipowaongoza kutwaa ushindi wa ligi ya Mabingwa.
Timu ya Manchester City inatamani ushindi huu ili kukamilisha mataji matatu ya kihistoria na hatimaye kuwapa taji moja ambalo wamekuwa wakilimezea mate kwa muda mrefu.
Mechi itaanza saa nne usiku saa za Afrika Mashariki, je ni nani atachukua kombe hili?