Vikosi vya Somalia viliwaua angalau wanamgambo 80 wa al-Shabaab, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa kundi, katika operesheni za kijeshi zilizotekelezwa kwa msaada wa washirika wa kimataifa, kulingana na shirika la habari la serikali.
Operesheni hizo zilifanyika katika maeneo ya Galmudug, Hirshabelle, na Southwest State katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
Hii inakuja siku chache baada ya kundi la kigaidi linalohusishwa na al-Qaeda kushambulia kambi ya kijeshi katika eneo la Lower Shabelle. Wanamgambo wake walitumia mabomu ya kujitoa mhanga kuvamia kambi hiyo. Wanajeshi saba wa Somalia, ikiwa ni pamoja na kamanda wa kambi, na wapiganaji 10 wa al-Shabaab waliuawa katika mapigano hayo.
Kundi hilo limekuwa likipigana kwa karibu miongo miwili, likilenga kuangusha serikali kuu ya Somalia.
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alitangaza mwezi Desemba mwaka jana juu ya azma ya serikali yake ya kumaliza al-Shabaab ndani ya mwaka mmoja.