Sukari Tanzania

Hii ni kuanzia, keki unayokata wakati wa bethdei, biskuti unazowanunulia watoto, maandazi unayofungulia kinywa asubuhi kabla ya kwenda kazini. Vyote hivi vinaongezwa utamu na sukari.

Sasa bidhaa hiii inapopanda bei au kuadimika sokoni, lazima vilio visikike. Sio majumbani tu, bali, hata migahawani, viwandani na kwa mama lishe.

Hali hii imeikumba Tanzania hivi sasa. Katika miezi kadhaa iliyopita, kwanza kabisa, sukari ilianza kuadimika madukani, na pole pole bei kupanda kutoka ile ya kawaida ya shilingi 2700 kwa kilo hadi kufikia shilingi elfu 4 katika baadhi ya maeneo.

Tanzania ina jumla ya viwanda saba vya sukari, na kwa jumla, viwanda vyote vinatakiwa kuzalisha zaidi ya tani 1500 kwa siku, ili kukidhi mahitaji ya nchi ambayo ni sawa na tani 1500 kwa siku. Lakini serikali imesema, hivi sasa uzalishaji umepungua na kufikia chini ya tani 1000 kwa siku.

Athari za kukosekana kwa sukari zimeanza kuonekana kwa watu binafsi na hata wafanyabiashara wakubwa, ikiwemo baadhi ya viwanda ambavyo vimesitisha uzalishaji.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania, kupitia Bodi ya Sukari (SBT) imetoa Amri ya Bei Elekezi ya sukari nchi nzima.Kulingana na tangazo hilo, bei ya jumla kwa maeneo mengi ya nchi hiyo itakuwa kati ya Shilingi za Kitanzania 2,600 hadi 2,900 huku upande wa rejareja, bidhaa hiyo itanunuliwa kuanzia shilingi 2,700 hadi 3,200.Lakini je, serikali imechukua hatua gani kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo, hatua hii imeanza kulalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara, ambao wanasema, bei iliyotangazwa haiendani na bei waliyonunulia.

Hii sio mara ya kwanza kwa Tanzania kukabiliwa na tatizo la uhaba wa sukari nchini. Na mara kadhaa, kama hatua ya dharura ya kukabiliana na tatizo hilo, imekuwa ikitoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje. Hatua hii mara nyingi huibua hisia mseto. Je, wewe unadhani nini kifanyike kutatua tatizo la uhaba wa sukari nchini.

TRT Afrika