Mwaka mwingine, kampeni nyingine. Siku ya Kimataifa ya Wanawake tarehe 8 Machi ya kila mwaka huja na kuondoka lakini kuna hofu sasa kwamba inaanza kuwa siku nyingine tu kwenye Kalenda.
Aidha uchovu wa kampeni au mchanganyiko wa kipaumbele, wanaharakati wanahofia kuwa masuala ya wanawake yataanza kuponyoka kwenye mianya kama kasi hiyo haitadumishwa au hata kuongezwa.
‘’Watu wanaanza kufanya mambo kwa uchache tu kiasi cha kusalia kuwa sahihi kisiasa kuhusu haki za wanawake na kusherehekea tu Kalenda, kisha wanasahau,’’ anasema Terry Anne Chebet, mwanahabari nchini Kenya na mwanzilishi wa shirika la Leading Ladies la Afrika.
‘’Tunahitaji kushika kasi kwa sababu kwa kadiri tulivyopiga hatua kubwa bado haijafanywa ya kutosha ili kumweka mtoto wa kike kwenye jukwaa sawa na wavulana,’’ anaiambia TRT Afrika.
Siku ya Kimataifa ya Wanawake huleta ulimwengu pamoja kusherehekea mafanikio na michango ya wanawake kote duniani.
Mwaka huu, mada "Wekeza kwa Wanawake" inalenga kutoa wito wa kuzingatiwa zaidi kwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani kote.
‘’Ningeifananisha hiyo na ‘Greenwashing’ katika harakati za mabadiliko ya Tabianchi,’’ Terry Anne anaiambia TRT Afrika.
‘’Ni kati ya mambo mazuri ya kufanya, lakini si uwekezaji wa kweli kwa wasichana na wanawake. Kwa mfano ukienda ngazi ya jamii, ndio utaona elimu inafunguka lakini unadhani nani atakuwa wa kwanza kung’olewa au kuachishwa masomo ikiwa familia inatatizika kupata ada? Ni kama kuwa ili mtoto wa kike apate haki yake, lazima kwanza mtoto wa kiume apate shibe yake,’’ anaelezea Terry Anne.
Upatikanaji sawa wa elimu na mafunzo
Uwezeshaji wa kiuchumi ndio kiini cha mada ya 2024. Kulingana na Umoja wa Mataifa kuhusu haki za Wanawake, UN Women, njia pekee ya kuondokana na mzunguko wa umaskini katika jamii yoyote ni kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Watasaidia familia zao, na kuchangia ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema wanawake wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vingi vya ushiriki wa kiuchumi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa elimu, rasilimali fedha, na nafasi za kazi. Na Terry Anne anakubali.
‘’Ikiwa ulitafuta neno pesa mtandaoni, 90% ya picha zitakazojitokeza ni pesa mikononi mwa wanaume,’’ anasema.
‘’Ni kana kwamba wanawake bado hawaaminiki vya kutosha au kutiwa moyo kuchukua usimamizi wa uwekezaji na uchumi wa jamii. Kuna hatua nyingi sana zilizopigwa leo, kuleta wanawake kwenye meza, lakini hata hailingani na kiasi bado tuko nyuma,’’ anaongeza.
‘’Kuwekeza kwa wanawake kunamaanisha kuwapa fursa sawa ya kupata elimu na mafunzo, pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa ujasiriamali na ajira. Kwa kuziba pengo la kijinsia katika nguvu kazi na kukuza uongozi wa wanawake katika biashara na viwanda, tunaweza kufungua uwezo mkubwa wa kiuchumi na kuendeleza maendeleo endelevu,’’ anasema Terry Anne.
Siasa na uongozi
Wanaharakati wanakubali kupigania usawa na haki kwa wanawake ni kukimbia marathon na si mbio kukimbia kasi, lakini wakati jamii haiendi kwa kasi sawa katika hili, sehemu moja daima itaburuza nyingine nyuma.
Terry Anne anasema wanawake zaidi wamekuwa wakijitokeza licha ya changamoto zinapokuwa zinawakabili.
‘’Angalia Kenya kama mfano halisi, tunaona wanawake wengi wakijitokeza kuwania viti katika uchaguzi. Lakini wengi wao wanabanduliwa hata kabla ya uchaguzi kufika,’’ anaiambia TRT Afrika.
‘’Inawachukua kuruka viunzi vya kila aina kupata tu tikiti ya kugombea, hata kwa kiti cha msingi zaidi cha kisiasa. Wanawake wana ufahamu zaidi na wako tayari kuchukua uongozi lakini wanalengwa au kutishiwa na wanaishia kuanguka tu,’’ anaendelea kusema.
Simulizi kwamba mengi yamefanywa kuwawezesha wanawake isitumike kukandamiza msukumo zaidi wa usawa.
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Wanawake, Mmoja kati ya wanawake 10 anaishi katika umaskini uliokithiri (10.3 %).
Ripoti hiyo ilisema zaidi, ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, ifikapo 2030, inakadiriwa 8% ya idadi ya wanawake duniani - wanawake na wasichana milioni 342.4 - bado watakuwa wanaishi chini ya dola 2.15 kwa siku.
Wanaharakati sasa wanatoa wito kwa serikali, mashirika na watu binafsi kuendeleza kampeni zao nje ya kalenda badala ya kuifanya kuwa tukio la mara moja kwa mwaka.
‘’Najua kuna maendeleo mengi yamefanywa, lakini njia rahisi ya kujua kama ni ya kweli au la, angalia siku za kalenda. Mada hizi zitaangaziwa kutakapokuwa na ukumbusho wa kimataifa. Lakini inahitaji kuwa mazungumzo ya kila siku, mwaka mzima,’’ Terry Anne anasema.