Rais mteule wa mkutano wa COP28 Sultan Al Jaber / Picha: AFP

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imeahidi kufanya uwekezaji wa dola bilioni 4.5 kama juhudi zake za kuimarisha miradi ya nishati safi barani Afrika.

Tangazo hilo limefanywa na Rais mteule wa COP28, Sultan Al Jaber siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa kwanza wa kilele wa tabianchi barani Afrika unaofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

"Mpango huo utaweka kipaumbele katika uwekezaji katika mataifa barani Afrika yenye mikakati ya wazi ya mpito, mifumo ya udhibiti iliyoimarishwa na mpango mkuu kwa minajili ya kuendeleza miundombinu ya gridi inayounganisha ugavi na mahitaji.'' Sultan Al Jaber alisema.

Al Jaber, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Teknolojia ya Juu nchini UAE, na Mjumbe Maalum wa tabia nchi, alisisitiza kuwa uwekezaji huo mkubwa utachukua wajibu muhimu katika kuendeleza miundombinu na miradi ya nishati safi barani Afrika, kuendeleza uvumbuzi, na kukuza maendeleo endelevu.

Vile vile, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa na kuhakikisha mustakabali wa kijani kwa wote.

Jaber, ambaye pia anaendesha msukumo mkuu wa mpango huo kabambe, aliongeza umuhimu wa kuendeleza rekodi ya kibiashara iliyothibitishwa na kuanzishwa na UAE yenye suluhu bunifu za kifedha.

Aidha, alielekeza ujumbe wa wazi kwa viongozi wa Afrika, akiwahimiza kuimarisha sera na mifumo ya udhibiti ambayo itavutia uwekezaji muhimu wa kudumu unaohitajika ili kuharakisha upelekaji wa ufumbuzi wa nishati safi na mbadala katika bara zima.

Mkutano wa 2023 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi au Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), unaojulikana kama COP28, utakuwa mkutano wa 28 utakaoandaliwa kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023, katika Jiji la Maonyesho, Dubai.

AA