Tume ya Kitaifa ya kuzuia Utakatishaji wa Pesa na kupambana na ufadhili wa ugaidi imetoa maamuzi yenye vipengele vinne dhidi ya mchezo wa kamari wa 1XBET.
Kwa mujibu wa taarifa ya tume hiyo, Serikali ya Somalia imeamrisha mabenki yote, kampuni zinazotoa huduma za pesa kwa njia ya simu na watu binafsi wanaotoa huduma za kifedha zinazohudumu nchini Somalia, kutotoa huduma kwa wateja wa kamari nchini humo.
Maamuzi hayo yaliafikiwa baada ya kamati kufanya mkutano wake kwenye makao makuu ya Wizara ya fedha nchini Somalia, huku nchi hiyo ikipiga marufuku michezo yote ya kamari na kampuni ya kamari ya 1XBET.
"Serikali ya Somalia inapiga marufuku mchezo wa kamari kwa jumla, ambao unakwenda kinyume na maadili ya dini ya Kiislamu na sheria za nchi." Kamati hiyo iliandika kwenye barua rasmi iliyotoa.
Aidha kamati hiyo imeongeza kuwa imebaini uwepo wa kampuni inayotoa huduma za mchezo wa kamari inayoitwa 1XBET unapelekea uharibifu wa mali za watu wa Somalia.
"Huduma za 1XBET ni kinyume cha dini yetu na sheria za nchi yetu, na imekuwa na athari mbaya zaidi kwa uchumi, utamaduni wa kijamii na usalama wa nchi, kwa hivyo ni huduma haramu." Iliongeza.
Imemaliza kwa kusema rasmi kuwa 1XBET imepigwa marufuku nchini humo na hivyo basi, hatua zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka amri hizo.
"Iwapo kuna makampuni au benki ambazo tayari zinatoa huduma kwa kampuni ya 1XBET, zinaagizwa kusimamisha mara moja huduma hizona kufungia akaunti zao mara moja kwa kuwasilisha ripoti kwa wakala wa ripoti ya fedha wa FRC." Kamati ilieleza.