Kampuni ya Safaricom Ethiopia ya kutoa Huduma za Kifedha ya Simu ya Mkononi, imeanza kutumika rasmi leo, miezi mitatu baada ya kupokea kibali ya utoaji wa Hati ya Malipo kutoka Benki ya Kitaifa ya Ethiopia.
Wateja wote wa Safaricom nchini Ethiopia sasa wanaweza kupata huduma za M-Pesa kama vile kutuma na kupokea pesa ndani ya nchi na nje ya nchi, kulipa wafanyabiashara, kununua muda wa maongezi, kuhamisha hadi akaunti zao za benki, na kutuma pesa kutoka kwa akaunti zao za benki hadi kwa M-Pesa yao.
“Tunafurahia mwanzo wa matumizi ya M-Pesa nchini Ethiopia na kuanza kutoa Huduma za Kifedha za Simu kwa wateja wetu ikiwa ni utoaji huduma kwa zaidi ya wateja milioni 51 katika mataifa saba barani Afrika,” Stanley Njoroge, Mkurugenzi Mtendaji wa Muda wa Safaricom Ethiopia alisema.
Safaricom, ilitunukiwa rasmi leseni ya uendeshaji wa huduma za mawasiliano mnamo Juni 2021 kupitia shirika la Global Partnership for Ethiopia kabla ya kuzinduliwa rasmi mnamo Oktoba 2022, katika Hifadhi ya Urafiki, Addis Ababa ambapo iliidhinishwa kuendesha huduma za kutuma pesa kwa simu nchini Ethiopia.