Ajay Banga ameteuliwa kama rais mpya wa benki ya dunia / Picha : Reuters

Ajay Banga Singh ameteuliwa kuwa rais wa benki ya dunia kuanzia tarehe 2, Juni 2023, kufuatia tangazo la kujiuzulu mapema kwa rais wa sasa David Malpass.

Uteuzi huo unafuatia pendekezo la rais wa Marekani Joe Biden, ambapo ulifuatia uchunguzi wa kina wa bodi ya usimamizi wa benki kabla ya kupitishwa.

Ajay Banga amewahi kuhudumu kama rais wa kampuni ya MasterCard ambapo alisimamia zaidi ya wafanyakazi 24000, na kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mashirika makubwa ya kibiashara na viongozi wa mataifa, uzoefu ambao unatazamiwa kumpa nguvu katika nafasi yake mpya.

Ikithibitisha uteuzi wake, benki ya dunia imechapisha katika mtandao wa Twitter kuwa ‘’Bodi ya usimamizi imeridhishwa na uteuzi wa bwana Banga na inatazamia utendakazi na ushirikiano wake katika kukabiliana na changa moto kubwa zaidi zinazokabili mataifa yanayostawi.’’

Miongoni mwa masuala muhimu katika sera za benki hiyo, ambayo bwana Banga anatarajiwa kuangazia ni ufadhili wa malengo ya maendeleo yanayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, jambo lililomponza rais anayeondoka David Malpass.

Banga, 63, alizaliwa nchini India japo ameshapata uraia wa Marekani, na anakuwa rais wa kwanza wa benki ya dunia asiye na asili ya Marekani tangu kuanzishwa kwake punde baada ya vita vya pili vya kidunia.

Ajay Banga atashikilia wadhifa wa rais wa benki ya dunia kwa kipindi cha miaka 5.

TRT Afrika