Benki Kuu ya Tanzania (BOT) itaanza kuondoa kwenye mzunguko, noti za zamani za shilingi ishirini(20), mia mbili (200), mia tano (500) na elfu moja (1000) ifikapo Januari 6, 2025.
Taasisi hiyo ya fedha pia, inalenga kuondoa noti za zamani za elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003.
Kulingana na taarifa yake kwa umma, BOT pia itaondoa kwenye mzunguko noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010.
Mchakato huo, ambao utaanza Januari 6 hadi Aprili 5, 2025, utahusisha ofisi zote za benki kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.
“Aidha, matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia Aprili 6, 2025,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa BOT, baada ya tarehe hiyo, mtu yoyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo, hazitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote pale duniani; na benki zote zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.
“Hivyo, Benki Kuu inatoa rai kwa wananchi wote wenye akiba ya noti hizo za zamani, kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi kilichotolewa,” taarifa ya BOT iliongeza.