Serikali ya Kenya imeanza mchakato wa kuwasaka wawekezaji binafsi kuendesha na kusimamia vituo vitano muhimu vya bandari vikiwemo Bandari za Mombasa na Lamu, eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu, Bandari ya Kisumu, na Bandari ya Uvuvi ya Shimoni.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Kenya, nahodha William K Ruto tarehe 6, Septemba 2023, Kenya ilitangaza mwaliko rasmi kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya maendeleo na uendeshaji wa bandari kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na umma.
Hata hivyo, mipango hiyo imevutia hisia mbalimbali baada ya viongozi waliochaguliwa kutoka maeneo hayo akiwemo Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir kutangaza kutounga mkono mipango hiyo.
"Nikiwa Bungeni, nilikuwa mtetezi wa Bandari ya Mombasa na nitasalia kuwa hivyo. Tukiwa viongozi wa Mombasa kwa mshikamano, tumekutana sote wakiwemo wabunge wa maeneo hayo na spika wa bunge la Mombasa na tunapinga uuzaji wa bandari yetu," Nassir alisema.
Kulingana na tangazo la zabuni la hivi karibuni, wawekezaji wamepewa hadi Oktoba 12 kuwasilisha zabuni zao kwa mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), kusimamia maeneo tisa ambayo yanajumuisha gati nambari 1-3 ya kituo cha shehena cha Lamu, eneo Maalum La kiuchumi la Lamu, gati nambari 11-14 ya Bandari ya Mombasa, na kituo cha kwanza cha shehena katika Bandari kuu ya Mombasa.
Aidha Kikundi cha wabunge waliochaguliwa kutoka maeneo ya Pwani Kenya, walifanya kikao wiki hii huku wakijadiliana na kutoa kauli moja ya kupinga juhudi za kubinafsisha bandari hizo.
"Isipokuwa Bandari hii, hatuna njia nyengine ya pato la kiuchumi hapa pwani. Tutatangaza msimamo wetu kwa jumla kuhusu ubinafsishaji wa Bandari baada ya kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali," alisema Danson Mwakasho, mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge kutoka Pwani.
Kenya inadaiwa kuendelea na mazungumzo na wawekezaji wa kimataifa ili kuwakabidhi usimamizi wa Bandari ya Lamu, lakini mpaka sasa, mustakbali wa usimamizi wa Bandari ya Mombasa haijabainika wazi.