Wakimbizi kutoka Sudan hadi nchi jirani ya Sudan Kusini wanaendelea kuongezeka.
Vita nchini Sudan vinaendelea tangu Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces.
Shirika la kutoa msaada wa kibinadamu la Norwegian Refugee Council linasema kufikia tarehe 28 Januari 2024, zaidi ya wakimbizi 528,000 walikuwa wamevuka katika maeneo ya mpakani mwa Sudan Kusini kupitia eneo la Abyei, Upper Nile, Unity, Kaskazini na Magharibi mwa Bahr El Ghazal.
"Hii ina maana kwamba zaidi ya asilimia 30 ya wakimbizi wote, wanaotafuta hifadhi, ambao asili yao ni ya Sudan Kusini walilazimika kuikimbia Sudan tangu vita vilipolipuka Aprili 2023 kwa ajili ya ulinzi katika mojawapo ya maeneo maskini zaidi duniani," Jan Egeland, katibu mkuu wa NRC amesema.
Na huku wakimbizi wakiongozeka ndivyo mahitaji yao yanaongezeka huku mashirika ya misaada yakisema rasilimali kutoka jamii ya kimataifa ni duni sana.
" Tunashangazwa na hali ya jamii ya kimataifa huku raia wengi wasio na ulinzi wakiuawa na kuhamishwa ndani na kutoka Sudan. Tunashuhudia kutozingatiwa kabisa kwa maisha ya raia na ukatili wa kutisha uliofanywa na wahusika kwenye mzozo." Egeland ameongezea.
Imani ya mzozo huo kupata suluhisho umedidimia baada ya uongozi wa Sudan chini ya jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kusimamisha uanachama wake katika Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD. IGAD ilikuwa imeanza juhudi za kuhimiza upatanishi kati ya Jenarali al Burhan na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, kiongozi wa kikundi cha Rapid Support Forces.