Zaidi ya watu milioni 3 Kenya wapata chanjo dhidi ya kipindupindu na polio

Zaidi ya watu milioni 3 Kenya wapata chanjo dhidi ya kipindupindu na polio

Kampeni zililenga utoaji wa chanjo kwa maeneo nchini yalioathirika na magonjwa haya
zaidi ya watoto milioni moja na laki nane wamepata chanjo cha polio/ picha ya wizara ya afya Kenya 

Wizara ya afya Kenya inasema imefanikisha kampeni zake zilizo zinduliwa hivi karibuni kote nchini zilizolenga kutoa chanjo kwa watoto.

" Kampeni zetu za hivi majuzi zimepata matokeo ya ajabu," wizara ya afya ya Kenya imesema.

Watoto milioni 1.95 walichanjwa katika kampeni ya polio, wizara imesema.

Awamu ya kwanza ya kampeni dhidi ya polio nchini, ilianza tarehe 24 had 28 Agosti.

Watoto waliopata chanjo ya polio wako chini ya miaka 5. Awamu ingine ya chanjo itakuwa kati ya Septemba na Novemba.

Polio ni ugonjwa gani?

  • Polio (poliomyelitis) huathiri zaidi watoto chini ya miaka 5. Hata hivyo, mtu yeyote wa umri wowote ambaye hajachanjwa anaweza kuambukizwa ugonjwa huo.
  • Virusi huenezwa na mtu mmoja hadi mwingine hasa kupitia njia ya kinyesi-mdomo au, mara chache sana, vitu kama maji yaliyochafuliwa au chakula
  • Dalili za awali ni homa, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika, ugumu wa shingo na maumivu katika viungo.
  • Hakuna tiba ya polio, inaweza tu kuzuiwa. Chanjo ikitolewa mara kadhaa, inaweza kumlinda mtoto maisha yake yote.
  • Inaweza kusababisha kupooza miguuni

Kampeni dhidi ya kipindupindu

Wizara ya afya inasema zaidi ya watu milioni 1.6 wamechanjwa katika kaunti nane za nchi.

Chanjo dhidi ya cholera ilitolewa kwa kaunti nane za Kenya/ Picha ya wizara ya afya ya Kenya 

Kaunti zilizopewa kipaumbele kwa chanjo hii ni zile zilizoathirika zaidi na kipindupindu.

"Serikali ina mpango wa kuzuia kipindupindu kupitia chanjo kwa njia ya mdomo kufikia mwaka 2024, na mpango wa kitaifa wa kuangamiza ugonjwa huu kabisa ifikapo mwaka 2030," wizara ya afya imesema.

Kipindupindu ni nini ?

  • Kipindupindu ni ugonjwa wa kuhara unaosababishwa na kula chakula au maji yaliyochafuliwa na bakteria ya Vibrio cholerae.
  • Kipindupindu inaweza kusababisha kuhara maji maji kwa papo hapo.
  • Ugonjwa huu unaweza kumuua mtu ndani ya masaa machache ikiwa haijatibiwa.

TRT Afrika