Zaidi ya kaya milioni 2.6 zimehesabiwa katika Sensa inayoendelea nchini Uganda ikiwa hii ni siku ya tano tangu mchakato huo kuanza.
Hi ni asilimia 30 ya kaya 8.7 zilizotengwa kuhesabiwa.
Ofisi ya Takwimu ya Uganda imekubali changamoto za awali za masuala ya kiufundi katika sensa hiyo, ikiyahusisha na watu walioingia mitandaoni bila idhini na ambao hawajaajiriwa.
"Tuna zaidi ya aina moja ya vifaa, hivyo mahali ambapo kuna shida ni katika vifaa vya ndani ya jiji la Kampala na mji wa Wakiso," James Kizza mkurugenzi wa dijitali ameelezea.
"Ni vizuri kuwa tuna sera ya makubaliano ya kubadilisha vifaa hivyo na kampuni iliyoitengeneza, kwa hivyo vilivyoharibika zinachukuliwa na kurudishwa na tunapata vyengine," ameongezea.
Wafungwa 70,000 waliowekwa katika vitengo vya magereza 269 vilivyowekwa katika mikoa 19 wamekwishahesabiwa.
Maswali ya sensa yanahusisha tabia za makazi na uhamiaji, taarifa za wazazi, hali ya ulemavu, elimu, kusoma na kuandika na fani ya utaalamu viashiria vya soko la ajira, uzazi na vifo vya utotoni na uhamiaji
"Kumbuka tunahitaji kufikia idadi ya watu ambao makadirio yao ni zaidi ya milioni 45. Wacha tushirikiane na timu ya Sensa, sote tutahesabiwa," Mamlaka ya Takwimu ya Uganda imesema katika taarifa mtandaoni.
Maswali mengine pia yanahusisha mali na ustawi wa kaya, umbali wa huduma za kijamii, shughuli za kilimo cha kaya, na vifo katika kaya.
Hii ni sensa ya sita ya watu kufanyika nchini Uganda tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1962. Kwa kawaida hufanyika baada ya kila miaka 10.