Afrika Kusini imerikuwa ikiongoza kwa visa vya mauaji duniani. /Picha: AFP

Zaidi ya watu 6,000 wameuawa nchini Afrika Kusini kati ya Aprili na Juni, takwimu za polisi zilionyesha, huku suala la kukabiliana na uhalifu lazidi kuwa sugu kwa serikali mpya ya mseto.

Waziri wa Polisi Senzo Mchunu alisema siku ya Ijumaa kuwa watu 6,198 waliuawa katika kipindi cha miezi mitatu, idadi hio imepungua kwa asilimia 0.5 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

"Idadi hii inasimulia hadithi ya kutisha, inayoonyesha uzito wa changamoto tunazokabiliana nazo," aliuambia mkutano wa waandishi wa habari Cape Town.

Ubakaji, katika nchi inayojulikana kwa uhalifu wa ngono dhidi ya wanawake na watoto, uliongezeka kwa asilimia 0.6, ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha miezi mitatu mwaka jana.

Nchi ilirekodi jumla ya ubakaji 9,309 kati ya Aprili na Juni.

Polisi pia walisema kulikuwa na uhalifu 44,735 unaohusiana na dawa za kulevya uliogunduliwa kutokana na hatua za polisi katika kipindi hicho.

"Tumetekeleza oparesheni kubwa zinazolenga makundi ya dawa za kulevya, na kusababisha kunaswa kwa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya," waziri alisema.

Idadi kubwa

Mwezi uliopita, Wamexico watatu na Waafrika Kusini wawili walikamatwa wakati vitengo vya polisi vya kijeshi vilipovamia maabara yenye thamani ya mamilioni ya dola iliyofichwa katika shamba la mbali kaskazini mwa Johannesburg.

Katika tukio tofauti, raia wa kiume wa Urusi alikamatwa pamoja na Mwafrika Kusini baada ya polisi kukamata mifuko 14 iliyojazwa kokeini yenye thamani ya randi milioni 252 (karibu dola milioni 14 za Marekani).

Uhalifu ni suala kuu linaloikabili serikali mpya ya mseto ya Rais Cyril Ramaphosa baada ya chama chake cha African National Congress kulazimishwa kuingia katika muungano na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance na vyama vingine vidogo kufuatia uchaguzi wa Mei.

"Nambari hizi zinawakilisha zaidi ya idadi kubwa; zinaonyesha hali halisi ya maisha ya wananchi wetu - hofu zao, hasara zao na matumaini yao ya kuwa na mustakabali wa salama," Mchunu alisema.

"Tutakabiliana na changamoto hizi ana kwa ana na kufanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kuwa Afrika Kusini ni mahali ambapo wote wanaweza kujisikia salama na amani kwa mara nyingine," aliapa.

TRT Afrika