Baada ya changamoto ya ugonjwa wa Ebola kukumba Afrika Magharibi mwaka 2014 na kuua zaidi ya watu 11,000, WHO ilitangaza kuwa itatayarisha orodha ya magonjwa hatari zaidi kupata kutokea duniani.
Mwaka uliofuata, Shirika hilo lilikuja na orodha yake ya kwanza na kusisitiza kuwa yatahitaji uangalizi mkubwa na wa haraka katika kupambana nayo.
Orodha ya awali ilijumuisha: Crimean Congo Haemorrhagic fever, ugonjwa wa virusi vya Ebola na Marburg, Lassa fever, MERS na SARS magonjwa ya coronavirus, Nipah na Rift Valley fever.
Miaka mitatu baadaye, WHO ilikuja na jina jipya; 'X'.
'X' ni ugonjwa gani?
Kwa mujibu wa WHO, japokuwa vimelea vya maradhi hayo bado havijulikani, ugonjwa huo unaweza kuwa janga lingine kubwa kimataifa.
Tangu kujumuishwa kwake katika magonjwa tishio duniani, WHO imetoa wito kwa viongozi wa kimataifa kuwa tayari kukabiliana na maradhi hayo.
Baada ya Uviko19, shirika hilo lilionya juu ya uwezekano wa ugonjwa mwingine mkubwa duniani.
"Hatupaswi kukabiliana na mambo bila kujiandaa; tunaweza kujiandaa kwa baadhi ya mambo yasiyojulikana pia," mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus aliwaambia viongozi wanaoshiriki katika Jukwaa la Uchumi Duniani, maarufu kama World Economic Forum, unaofanyika mjini Davos, nchini Switzerland.